NA GODFREY NNKO
SERIKALI kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imekuwa ikitenga zaidi ya shilingi milioni 250 kila mwaka kwa dhumuni la kuwahudumia wajasiriamali wadogo bila malipo yoyote nchini.
Hayo yamesemwa leo Aprii 15,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Dkt.Athumani Ngenya katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
"Sasa hivi mjasiriamali hasikuambie lolote kwamba TBS…sijui kuna nini, hapana kuna funds ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo.
“Hii inaonesha Mheshimiwa Rais anaangalia mpaka mjasiriamali mdogo aweze kuwezeshwa ili bidhaa yake iweze kupata ubora na iweze kuuzika ndani na nje ya nchi."
Amesema, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wana makubaliano kwamba, bidhaa yoyote ikitoka nchi fulani ikiwa na alama ya viwango inaruhusiwa kuingia nchi nyingine bila kufanyiwa vipimo nchi husika.
“Kwa hiyo, ili kuweza kuwainua wajasiriamali wetu Mheshimiwa Rais ametenga kila mwaka shilingi milioni 250 ili kuweza kuwainua wajasiriamali wadogowadogo hadi kufikia level ya kuweza kupata alama ya ubora.
"Ili walaji kwanza waweze kuwa na confidence wa ile bidhaa na kuinunia bila matatizo, lakini wewe pia mtayarishaji au msindikaji wa ile bidhaa awe na ile cofindece kwamba bidhaa yangu ni nzuri."
Amesema, hatua hiyo inampa mjasiriamali husika nafasi ya kupata soko pana katika ukanda wa Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Nichukue nafasi hii kwenu wanahabari hizi taarifa ziwafikie wajasiriamali ambao wanatamani bidhaa zao ziwe na alama ya ubora ziweze kuuzika kwa urahisi ndani na nje ya nchi,tuwaambie waje TBS funds zipo, Mheshimiwa Rais katoa funds sisi tutafuata taratibu zote kuanzia kwenda kuangalia sehemu yake anapozalishia, na kumsaidia kama haijakaa vizuri, hapa fanya hivi…
“Haitoshi, baada ya kuzalisha tutakwenda kuchukua sampuli yake bila malipo, tutakuja nayo maabara, itafanyiwa uchunguzi bila malipo, itapewa alama ya ubora bila malipo na baadaye ana miaka mitatu, bure kabisa kuweza kupata huduma za TBS.
“Na baada ya kupata alama ya ubora tunakuja mara mbili kwenye eneo lako la uzalishaji kuweza kuchukua sampuli kuhakikisha kwamba unaendelea na taratibu zile tulizokubaliana mwanzo wakati tunakupa ile lama ya ubora.
“Lakini pia, tunapita sokoni, gharama zote hizi zinalipwa na Taifa kwa ajili ya kusaidia kipindi cha miaka mitatu inakuwa ni bure,"amefafanua Dkt. Ngenya.
Mkurugenzi Mtendaji huyo ameelezea kwa kina kuhusu majukumu na mafanikio ya shirika hilo ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema, TBS ilianzishwa mwaka 1975 kwa juhudi za Serikali kama jitihada za kuimarisha miundombinu ya sekta ya viwanda na biashara ili kukuza uchumi wa Taifa.
"Kwa hiyo, shirika liliundwa kama miundombinu ya sekta ya viwanda na biashara ili kukuza uchumi wa Taifa hili."
Amesema, jukumu kuu la TBS wakati inaundwa ilikuwa ni kuratibu uandaaji wa viwango,lakini baadaye waliongezewa jukumu la kusimamia utekelezaji wa hivyo viwango.
Pia, amesema wanawajibika kutoa mafunzo kwa wenye viwanda na wazalishaji na utoaji wa huduma bora kwa kuzingatia viwango na kuvifanyia ugenzi vifaa vya vipimo.
"Fanikio la kwanza ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Kama mnavyofahamu huko nyuma miaka kama mitano, TBS ilikuwa iko tu makao makuu Dar es Salaam pale Ubungo, lakini taratibu sasa tumeweza kusogeza maana Tanzania ni kubwa, kuweka TBS hapa wakati inahitajika kule Kigoma haikuwa sahihi.
"Lakini, kadri muda unavyokwenda tunaweza kuona namna ya kuweza kujirekebisha, kwa hiyo kati ya mafanikio katika kutekeleza hayo majukumu ni hili.
"Tunajenga maabara katika mikoa ya kimkakati, katika hili shirika linatekeleza mradi wa makao makuu ya shirika wa maabara Viwango House pale Dodoma. Dodoma ni makao makuu ya nchi na ni mkoa wa kimkakati.
"Kwa hiyo tumeamua kusogeza huduma pale, tunajenga makao makuu, lakini kutakuwa na maabara lile jengo linaitwa Viwango House kama jina la taasisi lenye lilivyo."
Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, maabara hiyo itahudumia mikoa mitatu kwa maana ya Dodoma, Singida na Tabora."Itahudumia pamoja na mikoa mingine ya jirani pale kwa mfano Iringa."
Pia, amesema shirika hilo linatarajia kujenga maabara nyingine Kanda ya Ziwa ambayo itajengwa jijini Mwanza na nyingine jijini Arusha kwa Kanda ya Kaskazini.
"Maabara ya Kanda ya Ziwa inatarajiwa kuhudumia mikoa sita, Mkoa wa Mwanza wenyewe, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu.
"Mnafahamu mikoa ya kule ina mazao mengi sana, lakini pia ina biashara kubwa sana, kwa hiyo baada ya kujenga kwa mkoa wa kimkakati Dodoma makao makuu ambao umefikia asilimia 60 tunaendelea na ujenzi Mwanza ili kuweza kuhudumia Kanda ya Ziwa."
Amesema, kwa kufanya hivyo si tu kwamba watakuwa wamesogeza huduma karibu kwa wananchi bali kuwapunguzia wananchi wenye bidhaa zao gharama za kufika Dar es Salaam kuhudumiwa.
Kwa upande wa maabara ambayo inatarajiwa kujengwa hivi karibuni Arusha amesema, itahudumia Arusha yenyewe, Manyara, Kilimanjaro na Tanga."Na kiwanja pale tayari tumeshapata, bado ujenzi upo kwenye karatasi."
Vile vile amesema, katika kusogeza huduma karibu na wananchi wanaendelea kuimarisha ofisi zao za kanda.
"Shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ofisi zake saba za kanda ikiwemo ya Kaskazini ambapo makao makuu yapo Arusha.
"Kanda ya Kusini makao makuu Mtwara, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini makao makuu Mbeya, Kanda ya Magharibi makao makuu Kigoma.
"Kanda ya Ziwa makao makuu Mwanza, Kanda ya Kati makao makuu Dodoma, Kanda ya Mashariki kwa maana ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro."
Amesema, katika kipindi cha miaka mitatu wanefanya mambo makubwa kwa kutumia fedha za ndani na kusaidiana na wadau wa maendeleo.
"Shirika limeweza kufanya ununuzi wa vifaa vya maabara vya kisasa kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa bidhaa mbalimbali.
"Kwa kufanya hivyo tumeweza kuongeza wigo wa uchunguzi, lakini pia tumeweza kurahisisha uchunguzi na majibu yanapatikana mapema na kwa haraka zaidi."
Amesema, shirika lina maabara 12 ambazo zote zipo Ubungo. Maabara hizo zimehakikiwa na kupata cheti cha ithibati ya umahiri wa Kimataifa.