DODOMA-Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe Zainab Katimba amesema, katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali ilitenga Shilingi Bilioni 2.64 kwa ajili ya kugharamia taulo za kike ambapo kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 1.06 ni za ruzuku ya uendeshaji na Shilingi bilioni 1.58 ni fedha kutoka mapato ya ndani ya halmashauri.
Mheshimiwa Katimba ameyasema hayo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mheshimiwa Nora Mzeru aliyehoji nini mpango wa serikali kutenga bajeti kwa ajili ya taulo za kike mashuleni.
Amesema, hadi kufikia Machi, 2024 shilingi Bilioni 2.2 zimetumika ambapo pia wadau mbalimbali walichangia jumla ya Sh bilioni 1.5 na miradi ya shule ya elimu ya kujitegemea ilichangia shilingi milioni 119.5.
Mheshimiwa Katimba amezisisitiza halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya upatikanaji wa taulo za kike shuleni.