NA GODFREY NNKO
TUME ya Nguvu za Atomu Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission-TAEC) imesema,makusanyo ya maduhuli ya Serikali yameongezeka kutoka shilingi bilioni 8.7 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 10.9 mwaka wa fedha 2022/2023.
Hayo yamebainishwa leo Aprili 29, 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof.Lazaro Busagala katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Prof.Busaga amesema, mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kufungua ofisi za kanda, mipakani na kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
"Hii imechangiwa na Serikali kutengeneza mifumo ya TEHAMA, lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi."
Ameitaja mifumo hiyo kuwa, ni pamoja na Mfumo wa Malipo ya Leseni na Forodha (TANCIS),Mfumo wa Kielektroni wa Pamoja wa Uondoshaji wa Shehena Bandarini na Maeneo Mengine ya Forodha (TeSWS) na Mfumo wa Kieltroniki wa Nyaraka (EDMS) katika kutoa huduma.
Katika hatua nyingine, Prof.Busagala amesema, mafanikio mengine waliyoyapata ni kupunguza siku za utoaji wa cheti cha uchunguzi wa mionzi (RAC) kutoka zaidi ya siku saba hadi kufikia kwa wastani wa saa 3 hadi siku moja kwa asilimia 98.
"Awali utaratibu wa RAC ulikuwa una mlolongo mrefu ambao ulisababisha malalamiko mengi kutoka kwa wadau mbalimbali,"amefafanua Prof. Busagala.
Mbali na hayo amesema, Serikali ya Awamu ya Sita imeondoa tozo na kupunguza tozo kwa kuamua kubeba gharama za upimaji.
"Hii ni hasa kwa wale wanaosafirisha bidhaa nje ya nchi kwa kupunguza kutoka asilimia 0.2 ya malipwani kuwa asilimia 0.1 ya malipwani, sawa na punguzo la asilimia 50.
"Aidha, kwa wafanyabiashara wadogo hupatiwa huduma ya upimaji wa sampuli bure sawa na punguzo la asilimia 100."
Pia, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia kwa kuendelea kuiwezesha TAEC kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa kupitia sayansi ya teknolojia na nyuklia.
TAEC
TAEC ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003).
Sheria ya Bunge Na. 7(2003) ilifuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).
Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.
Ni kutokana na ukweli kwamba, teknolojia ya nyuklia inatumika katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kama vile afya, kilimo, ufugaji, viwanda, maji na utafiti.
TAEC imepewa jukumu la kupima mionzi kutokana na sababu mbalimbali, kwani licha ya kuwa na faida nyingi za mionzi, isipotumika inavyotakiwa ni hatari ikiingia katika mnyororo wa chakula kwa sababu inatoa nishati toka katika kiini cha atomu ambayo haiwezi kuharibiwa kwa aina yoyote ile.
TR
Licha ya TAEC kusimamiwa na Wizara ya Elimu, pia ipo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya Mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Afisa Habari Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao kazi hicho na TAEC leo.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya Umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya Sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa Ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) Ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.