Tanzania yaishauri WB kuweka vipaumbele katika miradi ya maendeleo Afrika

NA SCOLA MALINGA
Washington

TANZANIA imeishauri Benki ya Dunia (WB) kutilia maanani vipaumbele vya maendeleo vya nchi za Afrika ikiwemo kuzipatia fedha na ujuzi ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika la Benki ya Dunia) (WBG Africa Group 1 Constituency) ukiendelea, mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yenye kauli mbiu ya “Vision to Impact” inayoendelea jijini Washington D.C, Nchini Marekani. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF,Washington).

Rai hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB), kwenye Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika la Benki ya Dunia) (WBG Africa Group 1 Constituency) uliofanyika Washington DC, nchini Marekani.

Alisema kuwa, Benki ya Dunia imekuwa inasaidia kwa kiasi kikubwa nchi za Afrika na sasa wasaidie kuwekeza nguvu zaidi kwenye miradi ya Maendeleo ili kuinua uchumi kwa haraka.

“Tunaiomba Benki ya Dunia inapopitia matarajio yao iweke kipaumbele kwa Afrika na kwa nchi moja moja na kutoa nyongeza ya rasilimali fedha,” alisema Dkt. Mwamba.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (katikati) na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil (kulia), wakifuatilia Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika la Benki ya Dunia) (WBG Africa Group 1 Constituency), wakati wa mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoendelea jijini Washington D.C, Nchini Marekani.

Aidha, Dkt. Mwamba aliiomba Benki ya Dunia kupeleka fedha zitakazoongezwa kupitia mzunguko mpya wa Mfuko wa IDA 21 zipelekwe moja kwa moja kwa walengwa ili kupata matokeo chanya kwa haraka

Aidha, alitoa wito kwa Mashirika ya Fedha ya Kimataifa kutoa mikopo ya muda mrefu (Long Term Loans) isiyo na riba ili nchi za Afrika ziweze kutekeleza miradi ya maendeleo kikamilifu.

“Mikopo ya muda mfupi inaumiza nchi za Afrika, hivyo tunaomba mikopo iwe ya muda mrefu, miaka 50 hadi 70 na isiyo na riba,” alisisitiza Dkt. Mwamba.

Aidha, Dkt. Mwamba alitumia nafasi hiyo kuwakumbusha ombi la Serikali ya Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika uliofanyika Marrakech, Morocco mwaka jana, la kukifanya kiswahili kuwa miongoni wa lugha za mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo na kutumika kwenye mikutano mingine mingi ya Kikanda na Kimataifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (katikati), akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika la Benki ya Dunia) (WBG Africa Group 1 Constituency) uliofanyika Washington DC, nchini Marekani, wakati wa mikutano ya Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) inayoendelea jijini humo, ambapo alitumia fursa hio kuiomba Benki ya Dunia kutilia maanani vipaumbele vya maendeleo vya nchi za Afrika ikiwemo kuzipatia fedha na ujuzi ili ziweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. Kulia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil.

“Kiswahili kimekuwa moja ya lugha inayotumika katika mikutano ya Afrika Mashariki (EAC), SADC, AU na sasa inakwenda kupitishwa kutumika kwenye mikutano ya kimataifa,” alisema Dkt Mwamba.

Mkutano huo ulihudhuriwa na nchi 22 wanachama ikiwa ni pamoja na Tanzania, Botswana, Burundi, Eritrea, Eswatini, Ethiopia, Gambia, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Msumbiji, Namibia, Rwanda, Ushelisheli, Sierra Leone, Somalia, Sudan, Sudan ya Kusini,Uganda, Zambia, na Zimbabwe.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news