KAGERA-Upo umuhimu mkubwa kwa wananchi kuzitunza barabara pamoja na alama za barabarani ili kuzifanya barabara kuwa salama kwa watumiaji wakati wote, imeelezwa.
Hayo yamebainishwa na Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Ngara mkoani Kagera, Mhandisi Makoro Magori wakati akielezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhandisi Magori alisema ili barabara ziweze kuishi muda mrefu wananchi wanao wajibu wa kuzitunza na kuzilinda, hivyo kusaidia Serikali kuokoa gharama za matengenezo ya mara kwa mara.
“Kuepuka ajali za barabarani kila mwananchi anapaswa kulinda miundombinu ya barabara pamoja na alama zake ili watumiaji wa vyombo vya moto kuwa salama,” alisisitiza.
Kwa upande wa bajeti,Mhandisi Magori alisema kwamba katika kipindi cha miaka mitatu chini ya uongozi wa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ngara kwa mwaka 2023/2024 ilipata Shilingi bilioni 2.5 ukilinganisha na Shilingi bilioni 1.2 miaka ya nyuma.
Alisema, fedha hizo zimeweza kuboresha barabara za vijijini na mijini ambazo zimeweza kupitika wakati wote na kufungua uchumi wa wananchi na wilaya kwa ujumla.