TAWA yatoa misaada kwa waathirika wa mafuriko Rufiji

NA BEATUS MAGANJA

WANANCHI walioathiriwa na mafuriko wilayani Rufiji wameiona thamani na umuhimu wa uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) baada ya Aprili 16, 2024 kupokea misaada mbalimbali kutoka kwa taasisi hiyo.
Ni misaada yenye thamani ya shillingi millioni 20 ikiwemo tani 6.4 za unga wa sembe, Kilo 666 za maharage na magodoro 186.

Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA akimkabidhi misaada hiyo Mkuu wa Mkoa wa Pwani,Mhe. Abubakari Kunenge, Kamishna Msaidizi Mwandamizi,Abraham Jullu amesema TAWA imeguswa na janga la mafuriko lililowapata majirani na wadau namba moja wa uhifadhi wananchi wa Rufiji ambao wamehusika kwa kiasi kikubwa kulinda rasilimali za Hifadhi ya Selous na hivyo imelazimika kuwashika mkono.
Jullu amesema tangu changamoto hii ya mafuriko imejitokeza TAWA ilifika kwa haraka na kuongeza nguvu kwa kutoa kikosi cha Askari 24 ili kusaidia katika zoezi la uokozi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya mbinu za kujikinga na madhara yatokanayo na wanyamapori wakali na waharibifu hususani mamba na viboko kwa jamii ambapo mpaka sasa TAWA imetoa elimu hiyo kwa wananchi wapatao 4,225 na bado inaendelea na zoezi hilo.

Sanjari na hilo, TAWA imetoa boti moja lenye uwezo wa kubeba jumla ya watu 15 ili kusaidia katika shughuli za uokozi zinazoendelea wilayani humo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakari Kunenge amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupeleka misaada mbalimbali kupitia Serikali na Chama Cha Mapinduzi tangu wilaya hiyo ipate changamoto hiyo ya mafuriko.

Pia amewashukuru Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA Mabula Misungwi Nyanda kwa maamuzi ya haraka waliyoyafanya kupeleka misaada hiyo kwa wananchi wa Rufiji kwa wakati.
Mkuu huyo wa Mkoa ameendelea kuishukuru TAWA kwa msaada wa boti kwa ajili ya kufanya shughuli za uokozi na ushiriki wao wa ujumla katika zoezi la uokozi kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali vya dola na kukiri kuwa wananchi wa Rufiji wanaona thamani na umuhimu wa uwepo wa taasisi hiyo mkoani Pwani.
Licha ya kuishukuru TAWA, Mkuu wa wilaya ya Rufiji Meja Edward Gowele amesema TAWA imekuwa na mahusiano na mashirikiano mazuri kati yake na uongozi wa wilaya yake ndio maana imekuwa rahisi kwao kuitikia wito wa kutoa msaada kufuatia janga lililoikumba wilaya hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news