NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Viwango Tanzaia (TBS) limesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suliuhu Hassan limefanikiwa kutoa gawio kwa Serikali shilingi bilioni 18.1.
Hayo yamesemwa leo Aprii 15,2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),Dkt.Athumani Ngenya katika kikao kazi na wahariri wakiwemo waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
"TBS pia tunatoa gawio kwa Serikali, mfano katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita tumeweza kutoa kwa Serikali gawio la shilingi bilioni 18.1,"amesema Dkt.Ngenya huku akifafanua kuwa, pia wamefanikiwa kupata mapato ghafi shilingi bilioni 237.
“Kwa hiyo hatuko nyuma, tunajua Serikali ina miradi mingi, mikakati ambayo inahitaji fedha kwa mfano mradi wa reli ya kisasa,bomba la mafuta, bwawa (Mwalimu Nyerere) ambalo sasa hivi tunapata umeme, kidogo sasa hivi tuna uhakika.
“Tunajua kwamba Serikali yetu ina miradi mingi, kwa hiyo pamoja na kidogo tunachopata basi tunataka asilimia fulani itusaidie kule kuhakikisha kwamba mambo hayalali,"amefafanua Dkt.Ngenya.
TR
Licha ya TBS kuwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara pia ni miongoni mwa taasisi na mashirika ya umma ambayo yanasimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR).
Afisa Mawasiliano Mwandamizi kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho kati ya TBS na wahariri chini ya uratibu wa ofisi hiyo leo.
TR ilianzishwa chini ya Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 418 ya Mwaka 1959 na Sheria ya Msajili wa Hazina Sura 370 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa.
Lengo la kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ni kusimamia uwekezaji wa Serikali na mali nyingine za Serikali katika mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi ya umma kwa niaba ya Rais na kwa ajili ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mnamo mwaka 2010 kulifanyika mabadiliko makubwa ya sheria ambapo moja ya mabadiliko hayo ilikuwa ni kuifanya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwa ofisi inayojitegemea kimuundo.
Vile vile, katika mwaka 2014 baada ya kufutwa kwa Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) ofisi ilikabidhiwa majukumu ya shirika hilo.