TMA yatoa ufafanuzi kupatwa kwa Jua leo

DAR ES SALAAM-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa kuhusiana na kupatwa kwa Jua tarehe 8 Aprili, 2024.
Hali ya kupatwa kwa Jua ni tukio linalohusisha kivuli cha mwezi kuangukia juu ya uso wa Dunia ambapo katika maeneo yaliyo ndani ya kivuli hicho Jua huonekana likifunikwa na Mwezi kwa kipindi cha saa chache.

Kuna aina mbili za kupatwa kwa Jua; kupatwa kwa Jua kikamilifu ambapo mwezi huzuia kabisa mwanga wa Jua kufika katika Dunia na aina ya pili, kupatwa kwa Jua Kipete, Mwezi huzuia sehemu tu ya mwanga wa Jua, hivyo kutengeneza umbo la pete ya mwanga wa jua angani.

Jumatatu ya Aprili 8, 2024, kunatarajiwa kutokea kwa tukio la kupatwa kwa Jua Kikamilifu. 

Tukio hili linatarajiwa kutokea upande wa Bara la Amerika ya Kaskazini kupitia Mexico, Marekani na Kanada. 

Aidha, tukio hili linatarajiwa kuanzia maeneo ya kusini mwa Bahari ya Pasifiki ambapo Mexico itakuwa nchi ya kwanza kufikiwa na kupatwa kwa Jua Kikamilifu mnamo majira ya saa 5:07 asubuhi kwa saa za Amerika. 

Njia ya kupatwa kwa Jua itaendelea kutokea Mexico na kuingia Texas, Marekani majira ya saa 7:40 mchana ikipita baadhi ya maeneo na kisha kuingia Kusini mwa Ontario, Kanada na kutoka Bara la Amerika ya Kaskazini kupitia pwani ya Bahari ya Atlantiki katika mji wa Newfoundland, Kanada, saa 11:16 jioni.

Kwa kawaida, sehemu ya Jua inayofunikwa na Mwezi wakati wa kilele cha kupatwa kwa Jua Kikamilifu itatofautiana baina ya eneo na eneo. 

Maeneo yaliyo ndani ya njia ya kupatwa kwa Jua Kikamilifu yataona kupatwa kwa Jua kwa kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na maeneo yaliyo mbali zaidi na njia hii.

Kwa kuwa Tanzania inaangukia katika eneo la mbali zaidi na njia hiyo, hivyo haitashuhudia tukio hilo. 

Aidha, kutokana na tukio hili kutokea mbali zaidi na nchi yetu, athari za moja kwa moja katika masuala ya kijamii na kiuchumi hazitarajiwi kuonekana hapa nchini.

Mamlaka ya hali ya hewa inaendelea kufuatilia na itatoa taarifa za mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza katika hali ya hewa kulingana na tukio hili la kupatwa kwa jua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news