Tukubali tukatae, Yanga hii mwendokasi

NA LWAGA MWAMBANDE

YOUNG Africans Sports Club (Yanga SC) katika siku za karibuni imefanya uwekezaji mkubwa.
Uwekezaji ambao umeivusha klabu hiyo yenye maskani yake maeneo ya Jangwani jijini Dar es Salaam kutoka kudharauliwa hadi kukubalika na kupendwa.

Ni kupitia uwekezaji huo ndipo anbapo wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wameshuhudia mafanikio makubwa kuanzia michezo ya Kitaifa na hata Kimataifa.

Mshairi wa kisasa,Lwaga Mwambande amebainisha kuwa, katika miaka miwili, klabu hiyo imefanya makubwa.Endelea;

1.Tukubali tukatae, Yanga hii mwendo kasi,
Zamani iikatae, ile miaka mkosi,
Huko chini ichakae, CAF pasipo kikosi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

2.Mwaka jana tunajua, ule wake mwendokasi,
Shirikisho kuinua, kombe ilikuwa chansi,
Kule mwisho kubutua, ndiko kulikotughasi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

3.Mayele lipoondoka, tukadhani hii nuksi,
Kwamba itapepesuka, kama mlevi msusi,
Kumbe inaimarika, japo magoli sisisi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

4.Feitoto naye yake, jinsi yalivyoighasi,
Na ile nafasi yake, kwa mpira wa mat
Mudathir mambo yake, Feitoto kitenesi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

5.Na mara tukasikia, na kocha hayuko nasi,
Ile Nabi kuishia, habari hiyo msosi,
Dua la kuku sikia, kwa mwewe halina kesi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

6.Gamondi kama mgambo, akachukua nafasi,
Sasa amekuwa wimbo, ile ya Yanga nafasi,
Yashinda na zake tambo, iko katika utosi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

7.CAF hii ya mabingwa, ni kama vile nuksi,
Au ndivyo ilipangwa, vichambo visiwe nasi,
Mtani alivyotingwa, ingeweza zua kesi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

8.Heko benchi la ufundi, kazi yenu mwendo kasi,
Wachezaji kama kundi, mnajua siyo desi,
Na viongozi mafundi, ni kweli siyo tetesi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

9.Sasa tuliza mpira, CAF mepigwa kipepsi,
Fanya jambo la busara, imarisheni kikosi,
Ufungaji unakera, mwakosa nyingi nafasi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

10.Tembeeni kwa kutamba, tumekiona kikosi,
Ila vichwa mkivimba, mwajitukana matusi,
Wengine waja kimwamba, mkatwe vipisipisi,
Hii miaka miwili, makubwa mmeyafanya.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news