Tunaendelea na uwekezaji mkubwa Sekta ya Usafirishaji Majini-Serikali

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Uchukuzi imesema,inaendelea na uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafirishaji majini, ambapo kwa kuanzia zaidi ya shilingi trilioni moja zimeelekezwa huko.
Naibu Waziri wa Uchukuzi,Mheshimiwa David Kihenzile ameyasema hayo leo Aprili 17, 2024 kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo, Prof Makame Mbarawa wakati akifunga Semina ya Usalama wa Vyombo vya Usafirishaji katika Kanda ya Afrika ambayo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Semina hiyo ya siku mbili iliandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), International Marinetime Organisation (IMO) na Interferry.

Lengo la semina hiyo ni kutoa fursa kwa wadau mbalimbali kujadili mbinu bora za kuboresha usalama wa vyombo vya usafiri majini barani Afrika.
"Kwa sasa, Serikali yetu inafanya uwekezaji mkubwa zaidi kwenye maji, tumeweka zaidi ya trilioni moja kwenye ununuzi wa meli.

"Zaidi ya bilioni 650 kwa ajili ya kujenga kiwanda cha meli pale Kigoma na kujenga meli ya kubebea mizigo tani 15,000 katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria,"Mheshimiwa Kihenzile amebainisha.

Pia, amesema wanajenga meli nyingine ya MV Mwanza,kukarabati meli za kutosha Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na Victoria.
Vile vile amesema, wanaendelea na utafiti katika Bahari ya Hindi ambapo wanataka nako kuweka meli za kutosha.

"Sasa tunapofanya uwekezaji mkubwa namna hii lazima kujifunza namna ya kuweza kulinda watu wetu wakiwemo watumiaji wa vyombo hivyo, pamoja na watu wengine ambao wamo katika maji hayo."

Amesema, jitihada hizo zinafanyika ikiwa ripoti ya karibuni ilionesha vifo vinavyotokana na ajali za majini ni vingi.

"Kwa hiyo, takribani nchi 17 zimeshiriki zikiwemo zaidi ya sita kutoka nje ya Afrika."

Semina hiyo ilijikita katika kujadili na kujengeana uwezo katika namna ya kuimarisha usalama katika usafiri wa majini ikiwemo bahari, maziwa na mito.
"Na hii ni kwa sababu watu wengine wanapoteza maisha baharini, kule Nyasa, hata Victoria na vyanzo vingine mbalimbali duniani.

"Kwa hiyo, wenzetu wa IMO kwa maana ya International Marinetime Organisation waneandaa semina hii kutujengea uwezo juu ya namna ya kuweza kukabiliana na ajali na kuimarisha ulinzi zaidi katika maji.

"Tunawashukuru sana wenzetu wa International Ferries pale IMO, lakini niwashukuru wenzetu wa TASAC.
"Kwa sababu TASAC wanahusika moja kwa moja, ndiyo wamekasimiwa jukumu la ulinzi na usalama katika maji yetu, lakini wanakwenda mbele zaidi wanahusika pia na uhifadhi wa mazingira, kwa sababu inaweza kuwa ni ulinzi wa binadamu.

"Lakini, ukichafua mazingira unaathiri ulinzi na usalama wa viumbe hai, kwa hiyo imekuwa ni semina nzuri washiri zaidi ya 85 wameshiriki."

Katika hatua nyingine,Mheshimiwa Kihenzile kwa niaba ya Waziri Profesa Makame Mbarawa ametoa rai kwa watumiaji wa bahari, maziwa na maji mbalimbali kuzingatia usalama majini.

"Kwanza kwa kuhakikisha vyombo vyao vina sifa,sio vibovu na vinaendeshwa na watu wenye utalaamu na wazingatie sheria na taratibu ambazo zimewekwa.
"Katika nchi yetu siyo kwamba unajiendea tu, zipo sheria za Kitaifa na Kimataifa. Lakini, pili niendelee kuwasii wenzetu wa TASAC waendelee kusimamia ipasavyo namna ya kuweza kuimarisha ulinzi na tatu Serikali yetu imeendelea kujenga miundombinu ya kuweza kufuatilia usalama kwenye maji.

"Kwa mfano Ziwa Victoria mwaka jana tulisaini mkataba wa Ambulance inayotembea majini. Ambulance ambayo ina vifaa vyote kama kituo cha afya ili ikimkuta mtu pengine amekosa uokoaji inakwenda kumuokoa na hivyo kuimarisha usalama majini.
"Lakini, pia tuendelee kuimarisha usalama kwenye maji kwa sababu maharamia pia, wanatumia majini kufikia ajenda zao.

"Tukishirikiana sote litakuwa jambo jepesi kuweza kuimarisha usalama wa nchi yetu na kwa vyombo vyetu vya usafiri majini ili pawe mahali pema kwa shughuli zetu za uchumi kusaidia wananchi wetu,"amefafanua Mheshimiwa Kihenzile.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news