ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka Waislamu kuendeleza mambo mema waliofanya katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani hata baada ya kumalizika kwake.
Akizungumza katika Baraza la Iddi el fitri huko katika ukumbi wa Polisi Ziwani amesema,namna bora ya kubainisha kufuzu katika mafunzo yaliopatikana katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni kuyaendeleza mafunzo hayo katika maisha ya kila siku.
Amewataka kuendelea kudumu kufanya mambo ya kheri na kuacha mambo yote maovu kwani Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala ameusifia kuwa umma bora kutokana na kuamrishana mambo mema na kukatazana mabaya.
Aidha,Alhaj Mwinyi amewashukuru masheikh na walimu kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuendesha darsa katika misikiti, mihadhara mbali mbali na kutoa mawaidha kupitia vyombo vya habari kwa madhumuni ya kukumbusha juu ya maamrisho ya Mwenyezi Mungu ili kuweza kuzitakasa na kuzikuza imani jamboa ambalo limewezesha kufanya ibada kwa unyenyekevu na utii mkubwa.
Hata hivyo, amewataka kudumisha suala la amani na utulivu ili nchi iweze kupata maendeleo kwani bila ya amani na utulivu hakuna maendeleo yatakayopatikana.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala bora Mhe Haroun Ali Suleiman amesema Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amefanya mambo mengi mazuri katika kuwatumikia wananchi wake.
Hivyo ni vyema kumuombea dua kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema sambamba na kuiombea nchi kuwa na amani na utulivu.
Mapema Ustadhi Ismail Kassim Iddi kutoka chuo cha Kiislamu Mazizini amewasihi wananchi kuwatii viongozi wao kama misingi ya dini inavyotaka sambamba na kushiriki katika harakati mbalimbali za maendeleo ili Serikali kuweza kufikia maendeleo iliojipangia ya kutatua matatizo ya wananchi katika maeneo yao.