NA GODFREY NNKO
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko amesema, katika mwaka wa fedha 2023/24 Serikali iliendelea kuchukua hatua za kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa umeme nchini.
Dkt.Biteko amesema,hadi kufikia Machi, 2024 uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa ulifikia jumla ya MW 2,138 ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.2 ikilinganishwa na MW 1,872.1 za Mei, 2023.
Ameyasema hayo leo Aprili 24, 20024 wakati akiwasilisha bungeni jijini Dodoma hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati amefafanua kuwa, katika kiasi hicho MW 836.3 sawa na asilimia 39.1 ni umeme unaotokana na nguvu ya maji, MW 1,198.8 sawa na asilimia 56.1 gesi asilia.
Aidha, MW 92.4 sawa na asilimia 4.3 ni mafuta mazito na MW 10.5 sawa na asilimia 0.5 ni kutokana na tungamotaka (biomass).
"Ongezeko la uwezo wa uzalishaji wa umeme limetokana na kuanza kwa uzalishaji wa umeme katika Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (MW 2,115) ambapo MW 235 zimeanza kuzalishwa kupitia mtambo Namba 9.
"Pamoja na kukamilika kwa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Rusumo ambao unachangia MW 26.7 katika Gridi ya Taifa,"amefafanua Dkt.Biteko.
Dkt.Biteko amesema, hadi kufikia Machi 2024, uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme ambayo haijaungwa katika Gridi ya Taifa ni MW 33.4 ambazo zinajumuisha mitambo inayomilikiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yenye uwezo wa kufua MW 28.4 na MW 5 zitokanazo na nguvu ya jua kutoka kwa mzalishaji binafsi.
Vile vile, amesema wizara kupitia TANESCO inanunua umeme wa MW 31 kati ya hizo MW 21 kutoka Uganda kwa ajili ya Mkoa wa Kagera na MW 10 kutoka Zambia kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa.
Amesema, pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme katika kipindi cha Julai, 2023 hadi Machi 2024, bado uzalishaji huo ulikuwa haukidhi mahitaji ya nchi ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi.
Dkt.Biteko amesema ni kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii pamoja na changamoto za upungufu wa maji na gesi asilia katika vituo vya kufua umeme, hitilafu katika mitambo ya uzalishaji pamoja na kufanyika kwa matengenezo katika mitambo ya uzalishaji wa umeme.
"Mahitaji ya juu ya umeme nchini yamekua na kufikia MW 1,590.1 zilizofikiwa tarehe 26 Machi, 2024 saa 3.00 usiku sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ikilinganishwa na MW 1,470.5 zilizofikiwa tarehe 12 Juni, 2023 saa 2:00 usiku,"ameongeza Dkt.Biteko.
Kwa mwaka wa fedha ujao, Mheshimiwa Dkt.Biteko ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liidhinishe bajeti ya wizara hiyo ambayo ni zaidi ya shilingi trilioni 1.883 kwa ajili ya matumizi ya wizara na taasisi zake.
Dkt.Biteko amesema, kupitia fedha hizo,shilingi trilioni 1.794 sawa na asilimia 95.28 ya bajeti yote ya wizara ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Aidha, kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 1.54 ni fedha za ndani na shilingi bilioni 258.85 ni fedha za nje huku shilingi bilioni 88.89 sawa na asilimia 4.72 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
"Kati ya fedha hizo shilingi bilioni sitini na tisa, milioni mia tano ishirini na nne, mia mbili na moja elfu (shilingi 69,524,201,000) ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC)."
Ameongeza kuwa,shilingi bilioni 19.37 ni kwa ajili ya Mishahara (PE) ya watumishi wa wizara na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo.