Wachimbaji wadogo wazidi kuheshimishwa nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema, kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, wizara yake imeliwezesha Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kununua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo.

Amesema mitambo hiyo tayari imeanza kazi ya uchorongaji kuanzia Desemba 4, 2023 katika maeneo ya leseni za wachimbaji wadogo ya Nyamongo-Tarime, Itumbi-Chunya, Lwamgasa Geita, Katente-Bukombe, Buhemba-Butiama na Nholi Dodoma.
Mavunde ameyasema hayo leo Aprili 30, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Vile vile, Mheshimiwa Waziri Mavunde amesema, STAMICO inakusudia kufanya ujenzi wa vituo vipya viwili vya mfano vya kuchakata madini ya chokaa na chumvi.

Amesema, kituo kwa ajili ya kuchakata madini ya chokaa kitajengwa katika eneo la Kona Z Mkoa wa Tanga na kituo kwa ajili ya kuchakata chumvi kitajengwa katika eneo la Nangurukuru-Kilwa.

"STAMICO imeanza utekelezaji wa hatua za mwanzo za kuainisha mahitaji ya ujenzi wa vituo hivyo, kupitia vituo vya mfano vilivyopo Katente, Lwamgasa na Itumbi.

"STAMICO imeendelea kutoa huduma ya uchenjuaji wa dhahabu na kwa gharama nafuu kwa wachimbaji wadogo na kukusanya jumla ya shilingi milioni 794.13 katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024."

Aidha, amesema STAMICO imekifanyia maboresho Kituo cha Mfano cha Lwamgasa ili kuongeza uwezo wa kituo kuchenjua mbale ya madini ya dhahabu kutoka tani 9 hadi tani 30 kwa siku.

Katika kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za madini, Waziri Mavunde amesema,wizara na taasisi zake ilitoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo 10,213 kuhusu masuala ya usalama migodini, afya na utunzaji wa mazingira.

Waziri huyo amesema, wachimbaji hao walipatiwa mafunzo kuhusu biashara ya madini pamoja na ulipaji kodi na mirabaha ya Serikali.

"Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA) iliratibu ziara ya mafunzo kwa wachimbaji na wafanyabiashara zaidi ya 100 nchini China."

Amesema, katika ziara hiyo wachimbaji wadogo walipata fursa ya kutembelea viwanda vinavyotengeneza mitambo na vifaa vya uchimbaji 22 23 na uchenjuaji wa madini pamoja na kukutana na wafanya biashara wa madini wa China.

Mavunde amesema, ziara hiyo iliwawezesha wachimbaji hao kupata ujuzi, uzoefu na kujifunza kuhusu teknolojia mpya na kutafuta masoko ya madini.

"Wizara kupitia taasisi zake imeendelea kuwahamasisha wachimbaji wadogo kutunza kumbukumbu za uzalishaji na biashara za madini ikiwa ni moja ya vigezo vitakavyowawezesha kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.

"Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi, 2024 jumla ya shilingi bilioni 187 zilikopeshwa kwa wachimbaji ikilinganishwa na shilingi bilioni 145 zilikopeshwa kwa mwaka 2022.

"Nitumie fursa hii kushukuru benki za CRDB, NMB, AZANIA na KCB kwa kukubali kuwakopesha wachimbaji.

"Nitoe wito kwa taasisi nyingine za fedha zione umuhimu wa kuwakopesha wachimbaji kwa lengo la kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa tija,"amesisitiza Waziri Mavunde.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news