Washereheshaji waahidi kushirikiana na BoT kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za Tanzania

DODOMA-Wafawidhi wa Matukio (Washereheshaji) wa Chama cha Kisima Cha Mafanikio (KCM) wameahidi kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania katika kutokomeza utumiaji mbaya wa sarafu/fedha za Tanzania hususani kuzitumia kama mapambo katika sherehe mbalimbali za kijamii hapa nchini.
Hayo yamesemwa Aprili 4,2024 wakati wa mafunzo ya utunzaji mzuri wa fedha yaliyofanywa na Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Dodoma kwa Wanachama zaidi ya 250 wa KCM ambao wamejumuika katika mkutano mkuu wa mwaka unaoendelea katika ukumbi wa Kilimani jijini Dodoma.

“Sisi kisima cha mafanikio tunajitolea kuwa mabalozi wa hiari wa Benki Kuu na tunaahidi kutokomeza upambaji wa kutumia noti/fedha za nchi katika shughuli zote tunazozisimamia,” amesema Mwasisi wa chama hicho, Mwalimu Makena.
"Leo hii tumejua kwamba fedha zinatengenezwa kwa kutumia fedha za kigeni, hivyo matumizi yoyote yanayoenda kinyume na matumizi halali ya fedha zetu tutayakemea kwa nguvu zetu zote.”

Mwl. Makena amewaasa washereheshaji wote hapa nchini kuhakikisha matumizi ya noti zetu katika kupamba sherehe mbalimbali yanakoma.

Akitoa mada ya utunzaji unaofaa wa sarafu, Meneja Msaidizi Kitengo cha Sarafu Tawi la Dodoma, Bi. Matilda Luvinga, amewashukuru wanachama wa KCM kwa kuonesha nia ya dhati ya kuepusha hasara zinazosababishwa na matumizi mabaya ya fedha zetu.
“Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania inatumia gharama kubwa ya fedha za kigeni kutengeneza fedha zinazotumika hapa nchini. Benki Kuu ina wajibu wa kuhakikisha kuna fedha safi katika mzunguko muda wote hivyo uharibifu wowote ule wa fedha hauvumiliki,” ameeleza Bi. Luvinga.

Ametoa wito kwa wananchi wote kutunza fedha zetu vizuri ili gharama za kutengeneza fedha mpya zitumike katika shughuli nyingine za maendeleo kwa faida ya nchi kwa ujumla.
Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kuwaasa wananchi kuheshimu Shilingi ya Tanzania kwa kuwa ni moja ya alama ya taifa na kuonya kwamba kudhihaki na kukejeli noti na sarafu za nchi ni kosa la jinai.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news