ARUSHA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ambayo yatafanyika kitaifa mkoani Arusha.
Amesema hayo leo Jumanne, Aprili 30, 2024 wakati akikagua maandalizi hayo ambayo yatafanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
“Nimeridhishwa na maandalizi, niwatie shime tukamilishe sehemu iliyobaki, kesho tutakuwa wote, Waziri Mhe. Deogratius Ndejembi yupo na timu ya Ofisi ya Waziri Mkuu ipo hapa.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inaridhishwa na ushirikiano uliopo baina yake na vyama vya wafanyakazi nchini na itaendelea kuwajibika kwa yote muhimu yanayowaguswa wafanyakazi “tunazungumza pamoja na kukiwa na jambo lolote tunashirikishana, muelekeo wetu bado ni mzuri."

Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.