DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshuhudia utiaji saini mikataba 20 ya miradi ya umwagiliaji yenye thamani ya sh. bilioni 258.11 ambayo itatekelezwa kwa kutumia washauri elekezi na wakandarasi wa ndani na wa nje.
Mbali na miradi hiyo, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) kwa kutumia wataalam wa ndani, itatekeleza miradi minne yenye thamani ya sh. bilioni 16.95 kwa utaratibu wa Force Account ambayo itakapomilika, inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo.
“Kama tulivyoshuhudia, tayari tumekamilisha kusainiwa kwa mikataba ya utekelezaji wa miradi yote 14 ya ujenzi kwa kutumia wakandarasi yenye thamani ya shilingi bilioni 248.76. Vilevile, kuna miradi sita ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kutumia washauri elekezi yenye thamani ya shilingi bilioni 9.35,” amesema.
Ameyasema hayo leo Aprili 30, 2024 wakati akizungumza na washiriki wa hafla ya utiaji saini wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, wakuu wa Taasisi zailizo chini ya Wizara ya Kilimo na watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwenye ukumbi wa Mabele, jijini Dodoma.
“Nimefurahi kuona kuwa asilimia 82 ya wakandarasi waliosaini mikataba ni wazawa. Ninampongeza sana Waziri wa Kilimo kwa kusimamia suala hilo. Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa ili kutoa fursa na kuongeza ajira, ujuzi na kipato kwa wazawa.”
Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mahsusi za kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kwa kuelekeza nguvu kubwa katika kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo Serikali imeongeza bajeti ya fedha za maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
“Bajeti hiyo imeongezeka kwa asilimia 677 hadi kufikia shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/2024 ikilinganishwa na bajeti ya shilingi bilioni 46.5 iliyotengwa kwa mwaka 2021/2022. Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya uendelezaji wa miradi ya umwagiliaji nchini.”
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki hao, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema utiaji saini wa miradi hiyo unajumuisha hekta 129,792 ambazo zinahusisha ujenzi na usanifu na kwamba ikikamilika itasaidia kuongeza zaidi ya ekari 300,000 kwenye mtandao wa umwagiliaji.
Amesema, kwa sasa wizara yake imelenga kuvuna maji ya mvua kwa kujenga mabwawa makubwa mitano ili kuyahifadhi kwa muda mrefu na yaweze kutumika kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu Tume hiyo, Raymond Mndolwa, alisema katika kipindi cha mwaka 2022/2023 na mwaka 2023/2024, Serikali iliidhinisha sh. bilioni 361.5 mfululizo za kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi na ukarabati pamoja na upembuzi yakinifu wa miundombinu ya umwagiliaji.
“Katika mwaka 2022/2023, Tume ilipanga kutekeleza miradi 135 ambapo 69 kati ya hiyo ni ya ujenzi na ukarabati na 66 ni ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Katika mwaka 2023/2024, Tume ilipanga kujenga, kukarabati na kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika miradi 647.
“Utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji huchukua zaidi ya miezi 18, hivyo kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika skimu hizo kwa miaka hii miwili (2022/2023 na 2023/2024) kutaongeza eneo la umwagiliaji hekta 256,185.46 na kufanya eneo linalomwagiliwa kufikia hekta 983,465.46 sawa na asilimia 81.9 ya lengo la kufikisha hekta 1,200,000 ifikapo 2025.
Aidha, kuongezeka kwa eneo hilo kutatengeneza ajira za kudumu takribani 1,352,127,” alisema.
Akielezea kuhusu upatikanaji wa vitendea kazi, alisema Tume imefanikiwa kununua magari 48 kwa ajili ya watumishi, mitambo 15 na magari makubwa (heavy trucks) 17 kwa ajili ya usimamizi, ufuatiliaji na ujenzi wa miradi ya umwagiliaji.
“Tume imefungua ofisi 121 za Wilaya za Umwagiliaji na kuajiri watumishi 320 kwa ajili ya kusimamia miradi ya umwagiliaji katika ngazi ya Mikoa na Wilaya,” aliongeza.