Waziri Mkuu atoa maagizo kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi kuhusu michango ya wadau kwenye maafa

DODOMA-Waziri Mkuu Kasim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya waweke utaratibu wa kutoa taarifa za michango inayotolewa na wadau kwenye maafa ili kujenga imani kwao.

“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya ambao ni wakuu wa Kamati za Maafa kwenye maeneo yao watoe mrejesho ili kuweka uwazi na kujenga imani kwa wadau juu ya matumizi ya fedha zilizotolewa.”
Ametoa wito huo Bungeni leo Alhamisi, Aprili 18, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Agnes Hokororo kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inasimamia michango inayotolewa na inatoa mrejesho wa fedha zinazochangwa na wadau mbalimbali ili kukarabati majengo ya umma yaliyoharibiwa pindi majanga yanapotokea.

Waziri Mkuu amesema kwenye maeneo yoyote yanayokumbwa na maafa kama vile moto au mafuriko, zipo kamati maalum za maafa kuanzia ngazi za Kijiji, Kata, Wilaya na Mkoa ambazo zina wajibu wa kuratibu masuala yote ikiwemo misaada inayotolewa katika maeneo yao.

“Kamati hizi kwa ngazi za wilaya na mkoa huongozwa na Wakuu wa Wilaya na Mikoa wa maeneo husika. Hivyo wanao wajibu wa kutoa taarifa juu ya matumizi ya michango inayotolewa na wadau,” amesisitiza.

Akitoa mfano juu ya suala hilo, Waziri Mkuu aliyataja majanga ya kuungua moto soko la Moshi na Shule ya Sekondari Lindi kama baadhi ya maeneo ambayo yanatakiwa kutolewa taarifa za michango ya wadau ili wajue matumizi ya fedha zao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kusimamia kilimo na kuhamasisha wakulima wa mazao yote ya biashara na chakula ili waweze kulima kwa urahisi zaidi na kupata huduma kwa gharama nafuu.

“Sasa hivi tunatoa huduma hizo kwenye mbolea, dawa na zana za kilimo…, tumepunguza kodi kwenye vifaa vyote vya kilimo na hii ndiyo ruzuku ambayo tunaizungumzia. Tunapotoa ruzuku ya mbolea, mkulima anaweza kuitumia kwenye mazao yote,” amesema wakati akijibu swali la Dkt. Christine Mnzava (Viti Maalum) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kutoa ruzuku kwa mazao yote ya biashara ikiwemo zao la pamba.

Ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ruzuku ya sh. bilioni 50 kila mwaka kwa miaka miwili mfululizo ili zitumike kuagiza pembejeo ambazo zimesadia kuongeza uzalishaji wa mazao.

“Mwaka wa kwanza alitoa shilingi bilioni 50 na mwaka jana akatoa tena shilingi bilioni 50 ambazo tumenunua mbolea na dawa za kilimo na kutoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania.”

Mapema, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kupokea maoni na kufanya mapitio ya sheria zilizopo kuhusiana na masuala ya ukatili wa kijinsia ili jamii ibaki kuwa salama.

“Inawezekana makosa haya yanajirudia kwa sababu baadhi ya maeneo yana sheria lakini sheria zake si kali sana; na jambo hili ni mtambuka na linagusa wizara nyingi na kila wizara inaweka sheria zake katika kukinga jambo hili. Napokea ushauri wa kufanya mapitio kwani tunatamani kuona jambo hili likikoma kwenye jamii yetu.

“Niiase jamii yetu izingatie mila, desturi na tamaduni zetu ili tusiingie kwenye matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu kila mmoja na haki ya kuishi; kupunguza ulevi holela na kuacha imani potofu za baadhi ya makabila.”

Alikuwa akijibu swali la Tunza Malapo (Viti Maalum) ambaye alisema Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuangalia upya sheria zilizopo ama kuongeza adhabu ili kukabiliana na matukio ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo yanazidi kushika kasi katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news