Yanga SC mbioni kutwaa ubingwa Ligi Kuu ya NBC, Simba SC hali mbaya yapigwa mabao 2-1

DAR ES SALAAM-Pengine leo Aprili 20,2024 inakuwa siku yenye rekodi mbaya kwa Klabu ya Simba na mamilioni ya wafuasi wake ndani na nje ya nchi.
Ni baada ya wenyeji hao wa Mtaa wa Msimbazi kukubali kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa watani zao Yanga SC ambao ni wenyeji wa Jangwani jijini Dar es Salaam.

Mtanange huo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara umepigwa leo katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Stephanie Aziz Ki dakika ya 20 ndiye alianza kuzitikisa nyavu za Simba SC kwa mkwaju wa penalti, baada ya kuchezewa ndivyo sivyo na Hussein Kazi.

Kupitia kipindi cha kwanza katika dakika ya 38,Joseph Guede amepachika bao la pili akipokea pasi nzuri kutoka kwa Khalid Aucho.

Ushindi ulioifanya Yanga hadi mapumziko kuwa mbele kwa mabao 2-0 huku watani zao Simba SC wakiwa mbele kwa kumili mpira kwa ustadi mkubwa.

Simba Sc ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa Freddy Michael na kufanya matokeo kuwa 2-1 ndani ya dakika 90 ya mchezo.

Kwa matokeo hayo, Yanga SC inaendelea kubakia kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa alama 58 huku watani zao wakishika nafasi ya tatu kwa alama 46.

Ikumbukwe kuwa, Yanga tayari imecheza mechi 21 huku Simba ikiwa imecheza mechi 20,mwelekeo unaonesha Yanga SC wapo katika hatua nzuri ya kutetea ubingwa wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news