Ziara ya Kinana mkoani Mara yaibua mtifuano,Rorya ni pamoto

DAR ES SALAAM-Ziara ya Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Abdulrahman Kinana, anayotarajia kuifanya Aprli 14, mwaka huu imezua mtafaruku kwa makada wa chama hicho tawala wilayani Rorya.
Hali hiyo inatokana na uamuzi unaodaiwa kufanywa na viongozi wa chama na Serikali kuzuia makundi mengine kutomuona kiongozi huyo na kueleza hali ya mambo yanayoendelea kuelekea uchaguzi wa Serikali za vijiji, mitaa na vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

Kinana na msafara wake wanatarajiwa kuanza ziara ya kikazi Aprili 14, mwaka huu mkoani humo kwa lengo la kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi pamoja na kusikiliza na kutoa maagizo ya chama kuelekea uchaguzi.

Baada ya taarifa ya ziara hiyo, baadhi ya makada wa CCM wilayani Rorya wameibuka leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es Salaam na kueleza kero ambazo wanataka Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Bara kuzishughulikia anapokuwa wilayani humo.

Sambamba na kujua hali ya mambo yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa chama na Serikali wilayani humo.
Aliyewahi kuwa mtumishi wa CCM Makao Makuu idara ya SUKI, Baraka Otieno ambaye pia ni kada wa chama hicho wilayani Rorya amesema, kero kubwa ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya kuwagawa wanachama na viongozi wilayani humo.

Otieno amesema, pia baadhi ya viongozi wa CCM kutoka kata mbalimbali wamesimamishwa kazi kutokana na sababu ambazo hazijabainika na kuibuka makundi ya kikabila kwa kuwagawa wanachama wa CCM kwa Suba 1 na Suba 2.

Pamoja na hayo, Otieni alimtaja Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka na amedai kwamba ameshindwa kusimamia vyema suala la ulinzi na usalama na kusababisha mifugo zaidi ya 100 kuibiwa katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kwa mwezi Machi na April,mwaka huu.

Aidha, amedai imeibuka tabia ya kuachia wezi wanaokamatwa na kutotatua kilio cha wananchi wanaodai fidia kwenye shamba la mifugo la Utengi.

Kutokana na hali hiyo amemuomba Kinana kwenda na kusikiliza kilio cha wananchi hao na ikiwa viongozi wa CCM watashindwa kumueleza hilo yeye amejiandaa kukabidhi hoja hiyo kwa maandishi kwa kiongozi huyo wa CCM.

“Tunajua wakati haya yakiendelea na kupitia ziara hiii ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, tunapenda pia ajue Roya haina utulivu chama kinaendeshwa pasipo utaratibu ikiwamo viongozi kusimamishwa kisa tu hila za uchaguzi, chuki, ubabe wa Mwenyekiti, jambo hili si sawa sisi wana Rorya na wana CCM ni wajibu wetu kusema ukweli.

“Ukienda upande wa Serikali,Mkuu wa Wilaya Juma Chikoka, ameshindwa kusimamia kabisa suala la ulinzi na usalama watu wanaibiwa na hata kuporwa ng’ombe wao kwa nguvu na kuvushwa kwenda nchi jirani.
"Lakini hawana msaada wowote wa Serikali zaidi ya DC naye kujiingiza kwenye siasa hali ya kuwa si kazi yake.

“Rais Samia na wadau wa maendeleo wana mapenzi ya dhati na wilaya yetu ya Rorya, lakini bahati mbaya tumekosa viongozi wenye ubunifu na wenye kuwasaidia wananchi na badala yake wana kazi ya kubeba ajenda zao binafsi kuelekea uchaguzi na kuumiza watu,” amesema Otieno.

Kutokana na hali hiyo amesema kuwa, vitendo hivyo vinatokana na migogoro ya kisiasa inayoendelea sasa ndani ya Wilaya na Jimbo la Rorya.

MIGOGORO

Otieno amesema ,mivutano ya kisiasa imezidi kuwa mikubwa ikitawaliwa na ukanda na ukabila ambao umechagizwa kwa kiasi kikubwa na viongozi wa chama ngazi ya wilaya, ambapo mpaka sasa kuna kanda ikiwamo SUBA ‘one na two’ ambao ni ukanda unaodaiwa kuasisiwa na Mwenyekiti wa CCM, Ongujo Wakibar akidaiwa kushirikiana na mbunge.

Kutokana na hali hiyo alidai kuwa suala la makundi yakiwamo jamii inayozungumza lugha ya Kikurya na ambapo wanaishi kwenye Tarafa za Nyancha na Suba ambapo ilielezwa kuwa lengo la kundi hilo ni kuhakikisha wanaendelea kuzilinda kura za zinazodaiwa za mbunge ambapo kwenye kikao cha Machi 23, 2024 katika Shule ya Msingi Komuge walitoka na azimio hilo.

“Kundi la Girango na Luo-Imbo ni ni miongoni mwa makundi yaliyoundwa ili kuhakikisha mbunge aliyepo madarakani hapati nafasi tena kwa kinachosemekana ubaguzi wa wazi kwa watu wanaozungumza kiluo,”amedai.

Vile vile, Otieno amedai kuwa, kumekuwa na wimbi la viongozi wengi na wanachama wa CCM Rorya kufukuzwa na wengine kupewa onyo bila kutafutwa kwa chanzo cha tatizo.

Hali ambayo mpaka sasa inaendelea kuzua taharuki pamoja na kuwazuia wadau wa maendeleo katika utoaji wa misaada wilaya hiyo,jambo ambalo linafanywa na viongozi wa chama na Serikali ikiwa ni mkakati wao mahususi.

WIZI WA NG’OMBE

Akiyataja maeneo ambayo yanadaiwa kuibiwa ng’ombe na idadi kwenye mabano kuanzia Machi mwaka huu ni Nyambogo ng'ombe (4), Nyambogo ng'ombe (5) kwa kipindi cha Machi na Aprili.

Eneo lingine ni Ryagoro ng'ombe ambapo ng’ombe watatu waliibiwa Machi mwaka huu na wengine 6 Aprili , 2024.

“Ryagoro ng'ombe 6, Nyamware ng'ombe 10, Kitembe ng'ombe 6, Det ng'ombe 8, Bukwe ng'ombe 3, Malongo ng'ombe 3, Utegi ng'ombe 7 na Nyanduga ng'ombe 6,” amedai Otieno.

MWENYEKITI CCM

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Ongujo Wakibara alipotafutwa kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo alikanusha kuwapo kwa makundi kati ya Kata ya Subi 1 na Subi 2 pamoja na kuzungumza kilugha kwenye vikao vya chama licha ya kudai tarafa tatu kati ya nne kuzungumza lugha ya Kijaluo.

Kuhusu viongozi wa chama hicho waliosimamishwa kazi, alithibitisha kuwa ni wanne na hatua hizo zimechukuliwa na ofisi za CCM Mkoa wa Mara, baada ya wilaya kupeleka mapendekezo yaliyohusu makosa yao ambayo hata hivyo hakuyataja.

“Tunaomba Kinana anapofika Rorya kusikiliza kero za wananchi na wanachama wana kero ambazo viongozi wetu ndio wanaozifumbia macho na kuzuia kwa maslahi yao binafsi, tunataka waseme kama wataona ni sahihi kufanya hivyo,” amesema Wakibara.

Alipoulizwa suala la kusimaishwa kwa viongozi hao wa CCM hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa vijiji, mitaa na vitongoji haoni kama inaathiri mshikamano, alisema suala hilo ni la kawaida kwani chama kina timu kubwa ya watu ambao wanaweza kufanyakazi hiyo.

“Kwa mfano wewe ukiiba na ukasimamishwa kazi, kwani nafasi yako hakuna mtu wa kujaza…

"Sasa hilo si jambo la kushangaza ndani ya chama chetu. Sijasema kuwa wameiba ila wamesimamishwa kwa sababu ambazo uongozi wa mkoa unaweza kuzisema, lakini si mimi,” amesema Wakibara.

DC RORYA

Naye Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka akizungumzia kwa njia ya simu na waandishi wa habari, amesema suala la usalama wa mifugo ni tatizo linalotokana na wananchi wengi wa wilaya hiyo kushindwa kujenga mazizi na usalama mdogo wa mifugo na kukanusha kuachia mwizi wa mifugo kwa amri yake.

“Siwezi kumtetea mwizi, mwizi ni mhalifu tu. Mifugo inalala nje, imefungwa kamba laini na hakuna ulinzi ndio sababu inaibiwa.

"Tumeanzisha kampeni ya 'Ng'ombe Zizini' kama ni ng'ombe ni mmoja au wawili mfugaji aonyesha unapofugia, tumeanzisha na kampeni ya ulinzi shirikishi kila vijana saba kutoka katika kila kitongoji washiriki ili kumaliza tatizo hili,” amefafanua Chikoka.

Kuhusu suala la wananchi wa shamba la mifugo la Utengi kutolipwa fidia, alisema ni suala la kisheria na taratibu za kuwalipa zinafuata na hawawezi kufanya uamuzi wowote bila kufuata taratibu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news