DODOMA-Waziri wa Ujenzi,Mheshimiwa Innocent Bashungwa amekabidhiwa jogoo ikiwa ni ishara ya kumpongeza kwa juhudi kubwa za urejeshaji wa mawasiliano ya Barabara katika eneo la Tingi-Kipatimo na Barabara Kuu inayounganisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Zawadi hiyo imetolewa leo Mei 29, 2024 na Mzee Kimbwembwe kutoka Kijiji cha Somanga ikiwa saa chache kabla ya Bashungwa kuwasilisha bajeti yake bungeni kwa mwaka 2024/25.
Hata hivyo, Mzee huyo amesema kuna zawadi kubwa waliyomuandalia Rais wa awamu ya sita Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kutuma fedha nyingi za kurudisha miundombinu ilipoharibika lakini akasema hawezi kuitaja kwa sasa kwani hadi wakubaliane na wananchi wenzake.
Julai 30, 2020 Mzee Kimbwembwe alimkabidhi zawadi ya jogoo Rais wa awamu ya tano Hayato Dkt. John Pombe Magufuli alipopita katika eneo hilo ambapo alimshukuru kwa kuwapelekea kituo cha afya.
“Na wewe Bashungwa (Waziri wa Ujenzi) kwa kauli moja sisi wananchi wa Kilwa tumekuletea zawadi hii kutokana na kazi kubwa uliyoifanya kwa kurudisha mawasiliano ndani ya saa 72 kama ulivyoahidi,” amesema.
Mzee huyo amesema kilichowafurahisha wananchi wa huko ni kitendo cha Waziri kukaa huko kwa siku tano akishughulika na urudishaji miundombinu iliyokatika kwa sababu ya mvua kubwa jambo linaloonyesha kujali.
“Tunachojua ulifika pale kwa sababu ya maelekezo maalumu ya Rais wetu kipenzi Dkt Samia Suluhu Hassan, sisi wananchi wa Kilwa kuna zawadi tuliyomuandalia ambayo siwezi kuitaja leo maana sikutumwa hilo,kamwambie tunampenda na zawadi yake itamfikia,” amesema Mzee Kimbwembwe.
Akipokea zawadi hiyo, Waziri Innocent Bashungwa amesema zawadi aliyopewa imempa nguvu lakini akataka shukrani kubwa ziende kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani ndiye muwezeshaji wa mipango yote.