Arab League yakaribisha tangazo la Uhispania, Ireland kutambua taifa la Palestina

NA DIRAMAKINI

JUMUIYA ya Nchi za Kiarabu (The Arab League)
imekaribisha hatua za mataifa ya Uhispania, Ireland na Norway kuitambua Mamlaka ya Palestina kama taifa.
Katibu Mkuu wa Arab League, Ahmed Aboul Gheit. (AP/File).

Mawaziri wakuu wa nchi hizo tatu walisema Mei 22,2024 kwamba wangeitambua Palestina kama taifa kuanzia Mei 28,mwaka huu.

Ahmed Aboul Gheit,Katibu mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, amesema kwamba, "hatua hii muhimu inasisitiza dhamira ya kweli kwa suluhisho la serikali mbili na inaonesha hamu ya dhati ya mataifa haya ya kuilinda dhidi ya wale wanaotaka kuidhoofisha au kuitokomeza."

Gamal Roshdy, msemaji wa Aboul Gheit, amesema kwamba, “maendeleo haya muhimu yanafuatia utambuzi wa hivi karibuni wa Barbados, Jamaica, Trinidad na Tobago, na Bahamas.

"Ongezeko hili linaleta jumla ya idadi ya nchi zinazolitambua taifa la Palestina kufikia takribani 147, zikiambatana na makubaliano makubwa ya kimataifa."

Roshdy amesema utambuzi kama huo ni kipengele cha msingi cha msimamo wa serikali katika sheria za kimataifa.

"Hatua hii inajumuisha msimamo wa kisiasa, kimaadili, na kisheria wenye kanuni. Inaashiria hatua muhimu kuelekea kulitambua taifa la Palestina kwa kuzingatia mipaka ya mwaka 1967, Jerusalem Mashariki ikiwa mji mkuu wake,"amesema Abdul Gheit.

Vile vile, Aboul Gheit amesema kuwa, "kutambuliwa kunatoa ujumbe wazi kwa Wapalestina kuwa, ulimwengu unasimama kwa uthabiti katika kutetea haki yao ya kujitawala na kuanzishwa kwa dola huru."

Alisisitiza kuwa, "kati ya matatizo ya sasa, njia ya kisiasa inayoongoza kwa utambuzi wa taifa la Palestina haiwezi kuepukika."

Aboul Gheit alizitaka nchi ambazo bado hazijaitambua Palestina kutathmini upya misimamo yao na kujiweka sawa na historia.

Alisisitiza kwamba kutambua Palestina kunaashiria dhamira ya kweli kwa suluhisho la serikali mbili, kujitenga na mbinu za vurugu, na kuhimiza amani na usalama katika eneo lote.

Ukaribisho huo ulikuja muda mfupi baada ya Ireland,Uhispania na Norway kutangaza kwamba zitaanza kuitambua Palestina kuwa nchi kamili kuanzia Mei 28,mwaka huu.

Pia, mataifa hayo yamesema yanatarajia nchi nyingine za Magharibi zitafuata mkondo huo ili kurejesha amani katika ukanda huo.

Kutokana na uamuzi huo, Israel imekasirika na kuwaita mabalozi wake katika nchi hizo kurudi nyumbani.

Waziri mkuu wa Uhispania,Pedro Sanchez ameitaja hatua hiyo kuwa yenye lengo la kushinkiza kusitishwa vita kati ya Israel na wanamgambo wa Hamas huko Gaza.

Israel ilianzisha operesheni ya kijeshi huko Gaza kujibu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7,mwaka jana yaliyoua watu 1200 na kutekwa nyara watu 250.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, mashambulizi ya Israel katika eneo hilo yameua watu zaidi ya 35,000.

Uhispania imekuwa ikishawishi mataifa ya Ulaya yakiwemo Ufaransa, Ureno, Ubelgiji na Slovenia kuunga mkono juhudi za kuitambua Palestina kama taifa kamili.

Naye Waziri Mkuu wa Norway, Jonas Gahr Stoere amesema, hakuwezi kuwa na amani Mashariki ya Kati bila kuwepo suluhu ya madola mawili huru.

Ireland nayo kupitia Waziri wake Mkuu, Simon Harris imesema imechukua hatua hiyo iliyoitaja ya kihistoria kwa nchi yake na watu wa Paletina, kama njia ya kusaidia kupata suluhu katika mzozo wa Israel na Hamas.

Mbali na hayo, Kiongozi wa Palestina, Mahmood Abbas amekaribisha uamuzi huo na kuyataka mataifa mengine kuchukua hatua kama hiyo ili Palestina liwe Taifa kamili. (NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news