DODOMA-Wizara ya Afya inatambua kuwa huduma za Uuguzi na Ukunga ni mhimili muhimu katika utoaji wa huduma za afya hapa nchini ambapo asilimia 80 ya huduma za afya zinatolewa na wauguzi na wakunga.
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo bungeni Mei 13, 2024 akiwa anawasilisha hotuba yake ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/25 akielezea utekelezaji wa majukumu ya Wizara katika utoaji wa huduma za Kinga nchini.
"Tunatambua umuhimu wa Wauguzi na Wakunga ndio maana Wizara imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa kuwajengea uwezo watoa huduma ili kuweza kutoa huduma kwa kuzingatia utu, staha na mawasiliano madhubuti pindi wanapotoa huduma,"amesema Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy amesema, mpaka sasa jumla ya watoa huduma 6,544 katika Halmashauri 184 kutoka Mikoa yote 26 wamejengewa uwezo kuhusu utoaji wa huduma zenye staha na kuimarisha huduma kwa mteja (customer care).
Vilevile, amesema Wizara imeanza kuboresha vyumba vya kujifungulia ili kuweza kutoa huduma za mama mwambata ambapo mama anaruhusiwa kukaa na msindikizaji aliyemchagua wakati wa kujifungua.
"Jumla ya vituo vya kutolea huduma 42 katika Mikoa ya Katavi, Pwani, Kigoma, Dar es salaam pamoja na Morogoro vimeanza kutekeleza afua hii, Sambamba na hilo, Wizara imejengea uwezo watoa huduma 1,285 katika mikoa ya Mwanza,
"Shinyanga, Mara, Katavi, Geita na Dar es Salaam kuhusu matumizi sahihi ya chati uchungu ili kuendana na mapendekezo ya Shirika la Afya Duniani ya kuimarisha ubora wa huduma wakati wa kujifungua,"amesema Waziri Ummy.