DAR-Azam FC ya jijini Dar es Salaam imeibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Kagera Sugar kutoka mkoani Kagera.
Ni katika mtanange wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara uliopigwa Mei 25,2024 katika Dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Mabao ya Azam FC yamefungwa na Gibril Sillah dakika ya 50, Kipre Tiagori Emmanuel Junior Zunon dakika ya 65.
Wengine ni Feisal Salum Abdallah (Fei Toto) dakika ya 72 na 79 huku Iddi Suleiman (Nado) dakika ya 90 akimaliza kazi.
Kwa upande wa Kagera Sugar dakika ya 50’ walipata bao la kufuta machozi kutoka kwa
Mbaraka Yusuph.
Azam FC inafikisha alama 66 sawa na Simba SC na kuendelea kushika nafasi ya pili kwa faida ya wastani wa mabao katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Huku Kagera Sugar wakibaki na alama 31 katika mchezo wa 29 wakiwa nafasi ya 13 ambapo, ligi hiyo yenye timu 16, mbili zipo hali mbaya.
Mtibwa Sugar wanaburuza mkia kwa alama 21 wakifuatiwa na Geita Gold FC yenye alama 25 baada ya kila mmoja kukamilisha mechi 29.