DODOMA-Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Kilele cha Shindano la Kwanza la Vijana la Afrika kwenye masuala ya Akili Mnemba na Roboti (The African Youth in Artificial Intelligence and Robots Competition).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mohammed Khamis Abdula ameyabainisha hayo Mei 17, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Mheshimiwa Abdula amesema, shindano hilo litafanyika kuanzia Oktoba 13 hadi 17, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
"Tumekutana hapa leo hii, ili kupitia kwenu Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na Tume ya Tehama kutoa taarifa kuwa, nchi yetu Tanzania itakuwa mwenyeji wa kwanza wa kilele cha shindano la vijana barani Afrika kwenye masuala ya teknolojia zinazoibukia (emerging technologies).
"Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imepewa jukumu la kusimamia ukuaji na uendelezaji wa Sekta ya TEHAMA.
"Usimamizi huu unaendana na uanzishwaji wa sera, sheria, miongozo pamoja na mikakati mbalimbali inayohusu masuala na mabadiliko ya ukuaji wa TEHAMA itakayowezesha matumizi salama na yenye manufaa ya teknolojia zinazoibukia kama Akili Mnemba, robotiki na kadhalika."
Amesema, utekelezaji wa majukumu hayo umekuwa ukifanyika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta za umma, binafsi, mashirika ya Kitaifa na Kimataifa.
"Ili kujenga rasilimali watu endelevu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na taasisi zilizo chini yake imekuwa ikiandaa programu mbalimbali ikiwemo makongamano ya wataalamu wa TEHAMA ili kujadili masuala ya kuendeleza ujuzi wao katika eneo la teknolojia zinazoibukia Akili Mnemba, robotiki na kadhalika.
"Umoja wa Afrika (AU) umeandaa makakti wa kukuza matumizi sahihi ya Akili Mnemba, ambapo nchi mbalimbali zimekuwa zikishiriki katika kuandaa mkakati huo ambapo Umoja wa Afrika (AU-New Partnership for Africa’s Development) pamoja na Taasisi ya ELEVATE AI ni wadau wakuu wakioshiriki kuandaa makakati huo.
"Katika kutekeleza mkakati huo, nchi wanachama wanapaswa kuhamasisha ubunifu wa vijana kwenye masuala ya teknolojia zinazoibukia ikiwemo masuala ya akili mnemba.
"Napenda kuwajulisha umma kuwa mwaka huu 2024, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU) na Taasisi ya Ele Vate AI, imeanza maandalizi ya Kongamano la Vijana wa Afrika kuonesha bunifu zao na kushindana kwenye maeneo ya masuala ya Akili Mnemba,.
"Ambapo kumeandaliwa shindano linalohusisha vijana ambalo lilifunguliwa toka Februari 29, 2024 kupitia tovuti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya Tehama pamoja na tovuti ya www.ele-vate.co.za/competition ambapo shindano hili litafungwa tarehe Julai 8, 2024 na washindi watatangazwa Agosti 31, 2024."
Katibu Mkuu Abdulla amesema, maeneo ambayo yanashindanishwa ni;
i. AI and Innovation in Mining
ii. Futuurist FinTech Solution
iii. Robotics Design
iv. AI and Robotics Healthcare
v. Education Enhancemnennt
vi. Ethical AI
vii. AI and Robotics Agricultural Solutions
viii. Community Impact and Good Governance
ix. Innovations in Constructions and Artecture Industry
x. Open Category
"Ninapenda kuwajulisha kuwa washindi wa shindano hili, watakabidhiwa zawadi wakati wa Kilele cha Kongamano la Nane la Wataalamu wa Tehama Tanzania (TAIC) la mwaka 2024 litakalofanyika kuanzia tarehe 13 hadi 17 Oktoba,2024 nchini Tanzania.
"Kongamano hili litakuwa la kipekee tofauti na makongamano mengine yaliyopita na kutakuwa wananchi wataweza kuona roboti wengi ambao watakuwa wanaweza kujibu waswali mbalimbali.
"Ninawakaribisha Watanzania wote kuja kwenye kongamano hili na kuja kujionea matumizi ya Akili Mnemba.Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nichukue fursa hii kuwashukuru Umoja wa Afrika (AU), AU NEPAD na Taasisi ya Ele-Vate AI kwa kuona uwezo wa Tanzania kuwa mwenyeji wa kwanza wa maadhimisho ya kilele cha mashindano ya bunifu za Akili Mnemba.
"Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, tutatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha kuwa maadhimisho haya yanafanikiwa na kuwa mfano kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na Duniani kwa Ujumla.
"Kwa upande wa vijana wa Kitanzania, kampuni za ubunifu na jumuiya zinazohusika na masuala ya Akili Mnemba, natoa rai kushiriki kwa wingi kwenye shindano hili ili kudhibitisha utambulisho wa uwezo wa watanzania katika ramani ya wabunifu wa Akili Mnemba na roboti barani Afrika na duniani kote. TAZAMA VIDEO CHINI