Babati waomba Elimu ya Fedha iwe endelevu

MANYARA-Wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara, wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kuendelea kuwapatia elimu ya fedha kutokana na faida walizozipata baada ya kutembelewa na watumishi wa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI na kupatiwa elimu hiyo ya fedha.Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kupatiwa elimu hiyo katika shule ya Msingi Osterbay, wananchi hao wamesema kuwa, hapo awali hawakuwa na uelewa kuhusu matumizi sahihi ya fedha wanazozipata hali iliyosababisha wandelee kudidimia kiuchumi kutokana na matumizi mabaya ya kipato chao.

‘’Tunaomba Wizara ya Fedha, itoe elimu hii mara kwa mara kwa watu wote nchini,"amesema Bi. Anthonia Anthon.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Osterbay, Mwalimu Walter Ulotu, alisema kuwa elimu hiyo ya fedha itawasaidia watumishi wa umma hususani walimu wa shule hiyo waliopata fursa ya kushiriki katika mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya Fedha.

‘’Nimeona wajasiriamali ni wengi ambao wamehudhuria mafunzo haya kwahiyo tunaipongeza Wizara ya Fedha, lakini pia kwa kuwa yamefanyika hapa shuleni imeweza kutoa fursa kwa baadhi ya walimu wangu kujipatia elimu ya ujasiriamali na kuweka akiba na matumizi sahihi ya fedha binafsi,’’ amesema Mwalimu Ulotu.
Aliongeza kuwa, kutokana na umuhimu wa elimu ya fedha ni vyema Wizara ya Fedha ikaendelea kutoa elimu hii ili kuwasaidia wananchi kuelewa masuala mbalimbali ya kifedha ikiwemo kuweka akiba na matumizi bora ya fedha na kuandaa maisha ya kustaafu pamoja na maisha ya uzeeni.

‘’Pamoja na mambo mengine, lakini nimefurahia mada ya kujiandaa kustaafu, wengi wanakosa ile elimu ya fedha kwahiyo kiinua mgongo wanachokipata wanapostaafu hutumia vibaya, wengine hukimbilia kununua vyombo vya usafiri, ingependeza elimu hii itolewe mara kwa mara,"amesema Mwalimu Ulotu.
Naye Afisa Mkuu wa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa Wizara ya Fedha itahakikisha kuwa elimu ya fedha inawafikia Watanzania wote waliopo mjini na vijijini ili kuwapa uelewa wananchi kuhusu masuala ya fedha.

‘’Tunaendelea na programu hii katika mikoa mingine yote Tanzania, kwa awamu mbalimbali, lakini kwa awamu hii tulifanya kwa mikoa nane, lakini programu hii ni endelevu si kwa mwaka huu pekee, kila mwaka tutakuwa tunaendelea, lengo ni kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na elimu ya fedha na wanapata uelewa wa kutosha katika kufanya maamuzi sahihi ya kutumia huduma sahihi za fedha,"amesema Bw. Kimaro.
Elimu hiyo ya fedha ilianza kutolewa maeneo ya Mijini kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha kwa Mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza na Arusha, ambapo kwa sasa programu hiyo imejikita kuwafikia wananchi walio Vijijini ili kuwaongezea uelewa wa masuala ya Fedha ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mahitaji na matumizi ya Huduma za Fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news