Balozi Kasike ateta na Mjumbe wa Kamisheni ya Siasa FRELIMO
MAPUTO-Leo Mhe. Phaustine M. Kasike, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji amekutana na Mhe. Alcinda António de Abreu, Mjumbe wa Kamisheni ya Siasa ya Chama cha FRELIMO.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 20,2024 na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji.
Kupitia mkutano huo uliofanyika kwenye Ofisi za Makao Makuu ya FRELIMO zilizopo jijini Maputo, Viongozi hao wawili walizungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji na kukubaliana juu ya umuhimu kwa uhusiano huo kuendelezwa kwa maslahi ya nchi zetu mbili.
Kwa upande mwingine, Mhe. Balozi Phaustine alikipongeza Chama cha FRELIMO kwa kumaliza mchakato wa kumpata Mgombea wake wa nafasi ya Urais kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 09 Oktoba, 2024 ambapo Mhe. Daniel Francisco Chapo aliteuliwa kupeperisha bendera ya chama hicho.