Biharamulo wahamasishwa kuchangamkia Elimu ya Fedha

NA JOSEPHINE MAJULA, WF

MKUU wa Wilaya ya Biharamulo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Advera Bulimba, amewataka Wananchi wilayani Biharamulo kujitokeza kwa wingi ili wapate elimu ya fedha itakayowakomboa kiuchumi kwa ustawi wa jamii na nchi kwa ujumla.
Mkazi wa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, Bw. Duwa Juma, akiuliza swali kuhusu kiwango cha riba rasmi iliyowekwa na Serikali, kwa Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika wilayani humo kutoa elimu ya fedha ambapo iliwafundisha wananchi hao mada mbalimbali ikiwemo akiba na uwekezaji.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Kagera).

Rai hiyo imetolewa na SACP Bulimba, alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao wanaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Wilaya nne za Bukoba, Missenyi, Muleba na Biharamulo mkoani Kagera.
Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Advera Bulimba, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha (haipo pichani), ambayo ilifika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea njia watakazo tumia kufikisha elimu ya huduma ndogo za fedha katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.

“Katika wilaya yetu elimu hii ni muhimu sana kwa wananchi hawa, tatizo ni kubwa ilifika kipindi ilibidi niwapigie Benki ya Tanzania (BoT) ili wanisaidie hili jambo maana wananchi walikuwa wanateseka na mikopo yenye riba kubwa ambayo iliwafanya , wanyang’anywe mali na wadhalilishwe wakiwa maeneo ambayo hayafai kudaiwa,”alisema SACP Bulimba.

Alisema kuwa, nia ya Serikali ni njema kwa Wananchi wake hivyo ni muhimu Wananchi wa Wilaya ya Biharamulo wajitokeze kwa wingi kushiriki semina mbalimbali zitakazotolewa ili kupata elimu ya fedha ambayo itawasaidia kuepukana na mikopo yenye riba kubwa na kujiepusha na Taasisi zinazotoa mikopo bila kufuata utaratibu uliowekwa na Benki Kuu ya Tanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Advera Bulimba, akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha, ambao ipo mkoani Kagera kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha. Kutoka kushoto ni Afisa Mwandamizi Uchambuzi Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Gladness Mollel, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Biharamulo, Bw. Dirra Sila, Afisa Usafirishaji Wizara ya Fedha Bw. Rashid Bakari, Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bi. Mary Mihigo na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya.

Naye Afisa Biashara na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Biharamulo, Bw. Bahati Dominick, alisema kuwa katika Wilaya hiyo wananchi wa makundi mbalimbali wamefikiwa wakiwemo Watumishi, Taasisi za Fedha, Bodaboda, Wajasiriamali wakiwemo Mama lishe, Wanafunzi wa ngazi zote za elimu ya msingi, sekondari na vyuo.

“Katika wilaya yetu makundi karibu yote yamepata elimu ya fedha hii, hivyo kazi imebaki kwetu sisi waratibu kufuatilia iwapo elimu iliyotolewa imewafikia wananchi wengi kiasi gani ili tuweze kuboresha kwa awamu zijazo,”alisema Bw. Dominick.

Kwa upande wake mkazi wa Biharamulo, Bi. Tereza Nicodemu, alisema kuwa kupitia elimu aliyoipata amejifunza umuhimu wa kutoa taarifa za mikopo kama anaenda kuchukua mkopo kwa watu wetu wa karibu hususan ngazi ya familia.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakifuatilia maelezo ya mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wilaya hiyo.
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akielezea umuhimu wa kuweka akiba kwa wananchi wa Biharamulo wakati wa semina iliyotolewa kwa wananchi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wilayani humo.

“Tatizo la mikopo umiza imekua changamoto hata kwenye familia zetu hivyo ni vema mume au mke amshirikishe mwenza wake kabla hajaenda kuchukua mkopo ili wakati akishindwa kufanya marejesho mwenza wake aweze kumsaidia hii itasaidia kupunguza migogoro katika jamii,“alisema Bi. Nicodemu.

Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kbakaya, alisema kuwa Wizara imejiandaa vizuri kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia wananchi wengi wa makundi mbalimbali.

“Tumejipanga kama Wizara kuhakikisha tunafika mikoa yote ya Tanzania, lengo likiwa kila mwananchi aweze kuwa na elimu hii muhimu ikiwemo ya kuweza kuweka akiba kwenye njia rasmi, lakini pia aweze kupata elimu ya mikopo” alisema Bw. Kibakaya.
Afisa Biashara na Mratibu wa Huduma Ndogo za Fedha Wilaya ya Biharamulo, Bw. Bahati Dominick, akieleza umuhimu wa kukagua leseni ya usajili kwenye Taasisi za utoaji mikopo wakati wa semina iliyotolewa kwa wananchi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wilayani humo.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, walioshiriki semina ya elimu ya fedha, wakifuatilia filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wilayani humo.

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha katika mikoa ya Kagera, Singida na Manyara ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news