DODOMA-Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania imekusanya mapato kwa asilimia 77 ya mapato yote ya bajeti ya mwaka 2023/24.
Hayo yamebainishwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25.
Amesema,katika mwaka wa fedha 2023/24, Bodi ilipanga kukusanya shilingi bilioni 856.795 na kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 534,662,653,430 ni kwa ajili ya kugharamia kazi za barabara za Kitaifa ambazo ni Barabara Kuu na Barabara za mikoa zinazosimamiwa na Wizara ya Ujenzi.
Pia kiasi cha shilingi bilioni 254.6 zilitengwa kwa ajili ya kugharamia kazi za Barabara za wilaya ambazo husimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Waziri Bashungwa amesema,hadi mwezi Aprili 2024, Bodi hiyo imekusanya jumla ya shilingi bilioni 662.51 sawa na asilimia 77 ya bajeti ya mwaka.
Amesema,mgawanyo wa fedha hizo ni pamoja na Wizara ya Ujenzi ni shilingi bilioni 45.53, TANROADS ni shilingi bilioni 409.73, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Shilingi bilioni 20.097, TARURA ni Shilingi bilioni 180.87 na Shilingi bilioni 6.28 ni kwa ajili ya kugharamia shughuli za uendeshaji wa Mfuko wa Barabara.
"Bodi inaendelea kufanya ukaguzi wa ubora wa kazi za matengenezo ya barabara kwa kutumia wataalam wa ndani na nje ya taasisi ili kupata thamani halisi ya fedha katika miradi inayotekelezwa."
Bashungwa amesema, jumla ya miradi 562 ilifanyiwa ukaguzi kwa kutumia wataalam washauri na miradi 28 kwa kutumia wataalam wa ndani kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Aprili, 2024.