DODOMA-Serikali imesema kuwa,Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa leseni kwa kampuni mbili za kuchakata taarifa za mikopo, kampuni hizo ni Creditinfo Tanzania Limited na Dun & Bradstreet Credit Bureau Tanzania Limited.
Hayo yameelezwa leo bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Martha Nehemia Gwau, aliyetaka kujua idadi ya Kampuni za kutoa Taarifa za Mikopo (Credit Reporting Company) zinazoangalia hali ya kifedha ya mkopaji na uwezo wake wa kulipa hapa nchini.
Mhe. Chande alisema kuwa,Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006, imeipa Benki Kuu mamlaka ya kuanzisha na kusimamia kanzidata ya taarifa za wakopaji (credit reference system), kutoa leseni na kusimamia kampuni binafsi za kuchakata taarifa za mikopo (Credit Reference Bureaux).
‘‘Taasisi zote za fedha kubwa na ndogo zinatakiwa kupeleke taarifa sahihi Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo inasimamia kanzidata ya taarifa za wakopaji na kila baada ya mwezi taarifa hizo zinapokelewa na kusambazwa katika taasisi zinazohusika,’’ alifafanua Mhe. Chande.