DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo ya namna bora ya kutunza noti na sarafu zetu na uwekezaji katika Dhamana za Serikali kwa Baraza la Maridhiano la Mkoa wa Dodoma pamoja Washereheshaji kutoka Kisima cha Mafanikio (KCM) Kanda ya Kati katika ofisi za Makao Makuu ya Benki Kuu jijini Dodoma.
Siku ya kwanza ilikuwa ni kwa Baraza la Maridhiano la Mkoa wa Dodoma ambalo linaundwa na viongozi wa dini na siku ya pili kwa Washereheshaji.
Akizungumza mwanzoni mwa mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Taifa wa KCM and mwanzilishi, Mwl. Makena Bryson, alishukuru kwa mwaliko wa mafunzo hayo na kuitaka Benki Kuu iwe tayari kuitumia KCM kufikisha ujumbe kwa wananchi.
“KCM ni jumuiya ya washereheshaji wa kada mbalimbali katika matukio ya kijamii, wakiwa ni pamoja na washereheshaji, wapishi, wapambaji, na wapiga picha. Tumejiandaa vizuri kupokea mafunzo na kuanza utekelezaji mara moja,”alisema Mwalimu Makena.
Kutokana na mafunzo yaliyotolewa wakati wa mkutano mkuu wa KCM uliofanyika hapa Dodoma mwezi Aprili, KCM tayari wameanza kutoa elimu katika matukio wanayoyasimamia na mafanikio yanaonekana.
“Tumeshatunga hadi wimbo kuelezea kuhusu utunzaji mzuri wa fedha zetu. Ni vizuri ukikubalika uwe unatumika sehemu mbalimbali kuelimisha umma kuhusu suala hili muhimu,” alisema.
Mratibu wa mafunzo hayo kutoka Idara ya Mawasiliano Benki Kuu, Bw. Sadi Makomba, aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kwamba ni matumaini ya Benki Kuu kwamba elimu waliyoipata wataitumia kuwaeleza wateja wao na wananchi utunzaji mzuri wa fedha zetu na faida za uwekezaji katika dhamana za serikali.
Wakizungumzia mafunzo hayo, washiriki wengi walifurahia mafunzo hayo na kuahidi kuanza kuyafanyia kazi kwa vitendo kwa kuelimisha jamii kuhusu utunzaji mzuri wa fedha zetu pamoja na uwekezaji katika dhamana za serikali.
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
Habari
Mafunzo kwa Makundi Mbalimbali
Noti za Tanzania
Sarafu ya Tanzania