NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka Watanzania wote kila wanapofanya manunuzi au kupata huduma kuhakikisha wanadai risiti sahihi za Mashine za Risiti za Kielektroniki (EFD) na kama mtoa huduma hataki kufanya hivyo watoe taarifa kwa hatua.
Wito huo umetolewa leo Mei 29, 2024 na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano TRA, Bw.Hudson Kamoga wakati akifungua semina kwa wanahabari iliyoandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Jukwaa la Wanahabari wa Mitandaoni (JUMIKITA) jijini Dar es Salaam.
Kamoga amesema, makusanyo yanayokusanywa na Serikali kupitia kodi mbalimbali yamekuwa yakiwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hivyo kuifanya nchi kuwa tulivu wakati wote.
Amesema, katika kuhakikisha Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatekeleza mipango ya maendeleo fedha ni hitaji muhimu, hivyo suala la kulipa kodi ni lazima.
"Hivyo, sisi (wanahabari) ni wahamasishaji katika kulipa kodi, kwa sababu bila kulipa kodi,Mheshimiwa Rais atakuwa hana kitendea kazi, kwa hiyo kitendea kazi ambacho kinapeleka maendeleo ili kuhakikisha tuna barabara ambazo zinapitika vizuri, tuna miundombinu ya maji na watu wanapata maji safi.
"Tunapata elimu iliyo bora kwa maana ya miundombinu, kuhakikisha wanafunzi wa vyuo vikuu wanapata mikopo, tunaendelea kuimarisha shirika letu la ndege kwa maana ya kupata ndege.
“Ili kuweza kutekeleza hayo, Mheshimiwa Rais, kitendea kazi kikubwa ambacho anahitaji ni fedha, kwa hiyo sisi tukiwekeza katika kuhakikisha wananchi wanapata mwamko kwamba manunuzi yasifanyike bila kupata risiti.
"Kodi stahiki zitalipwa na mapato ya Serikali yatapatikana kwa ajili ya kufanikisha hayo,ndiyo maana tunasema dai risiti, kwa sababu ni haki yako,"amefafanua Kamoga.