DODOMA-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa ya Kulevya (DCEA) Kanda ya Kati Dodoma imekabidhi silaha mbili za moto kwa RPC wa Dodoma zilizokamatwa kwenye operesheni zilizofanyika tarehe 24 hadi 28 Aprili,2024 mkoani humo.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, leo tarehe 3 Mei, 2024 katika ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Kaimu Kamishna Msaidizi Kanda ya Kati, Mzee Kasuwi amesema, silaha hizo aina ya gobore zilikuwa zinamilikiwa na Hamisi Chambo (46) na Abdilah Juma (45) wote wakazi wa Kata ya Segera na zilikuwa zikitumika kulinda mashamba ya bangi.
Aidha, Kamishna Kasuwi amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kwa kupiga simu bure kupitia namba 119.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma (RPC) Theopista Mallya ameishukuru Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kutokomeza uhalifu na kutoa rai kwa wananchi kufuata sheria za nchi na taratibu zake kwani Jeshi la polisi lipo na litaendelea kutokomeza matumizi ya dawa za kulevya.
Tags
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Jeshi la Polisi Tanzania
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)