DAR-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Taasisi ya Care International kushirikiana na kuiunga mkono Tanzania katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo udhibiti na kukabiliana na maafa pamoja na kujenga uwezo wa mfumo wa tahadhari za mapema.
Makamu wa Rais ametoa wito huo wakati akifungua Mkutano wa Viongozi wa Kimataifa wa Taasisi ya Care International uliofanyika Hyatt Regency jijini Dar es salaam.
Amesema ushirikiano unaweza kuongezwa zaidi katika kujenga uwezo wa kustahimili mabadiliko ya tabianchi katika kuwezesha kilimo cha kisasa kinachoendana na hali ya hewa ili kuboresha tija na mavuno kwa wakulima wadogo.
Aidha,Makamu wa Rais amewasisitiza viongozi wa taasisi hiyo kuunga mkono Tanzania katika programu mbalimbali za kuinua wanawake kiuchumi ikiwemo matumizi ya nishati safi.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari amezindua Mradi wa Nishati Safi ya kupikia utakaowasaidia wanawake Barani Afrika (AWCCSP) pamoja na Kuzindua Mkakati wa Kitaifa wa nishati safi ya kupikia 2024-2034 ambapo ushirikiano na wadau unahitajika ili kulinda mazingira na kuokoa Maisha ya wanawake kutoka kutumia nishati isiyo rafiki hapa nchini.
Pia amewahimiza kuongeza ushirikiano katika kuwawezesha ujuzi wavulana na wasichana walionje ya mfumo wa elimu kwa lengo la kuwainua kimaisha na kuwajengea maendeleo mazuri ya baadae.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ushirikiano unahitajika katika tafiti na mipango ya namna ya kupunguza changamoto ya afya ya mama na mtoto inayozikabili nchi za kusini mwa jangwa la sahara. Ameongeza kwamba ni muhimu kufanyia tafiti suala la kuongezeka kwa kuzaliwa watoto kabla ya wakati (njiti) pamoja na suala la udumavu linaloikabili Tanzania licha ya kuwa nchi tegemeo kwa chakula.
Makamu wa Rais amesema kupitia juhudi za ushirikiano kati ya Serikali, CARE International na washirika mbalimbali, mafanikio makubwa yamepatikana kama ilivyoonyeshwa na viashirio muhimu vya maendeleo.
Amesema idadi ya watu wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wa mahitaji ya msingi imekuwa ikipungua kutoka 34.4% mwaka 2007 hadi 26.4% mwaka 2017-2018 na ilikadiriwa kuwa 25.7% mwaka 2020.
Ametaja kupungua kwa kiwango cha vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano kutoka vifo 81 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000 kati ya 2010 na 2022.
Idadi ya watu wanaopata maji safi na salama iliongezeka kutoka 74.5% hadi 79.6% vijijini na kutoka 86.5% hadi 90% maeneo ya mijini, kati ya 2021 na Februari 2024.
Kiwango cha uandikishaji shule za msingi na Sekondari kilifikia 92.7% na 89.1% mwaka 2024 na usawa wa kijinsia wa 1:1. Amesema hadi kufikia Februari 2024, vijiji 11,837 kati ya vijiji vyote 12,318 vya Tanzania Bara viliunganishiwa umeme, sawa na asilimia 96.1.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameipongeza Taasisi ya CARE Tanzania kwa kujikita katika kuwasaidia wakulima kuwezesha kufanya kilimo bora na uchakataji wa mazao hususani ya zao la chai.
Amewapongeza kwa kuwezesha ujenzi wa kiwanda cha mfano cha Uchakataji Chai cha Sakare kilichopo Korogwe mkoani Tanga na kuwezesha masoko kupitia mtandao.