Dkt.Mpango aziagiza Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI kuziwezesha Idara za Afya

PWANI-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango ameziagiza Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI kuziwezesha idara za Afya kuanzia ngazi ya Halmashauri za Manispaa, Miji na Majiji ili waweze kuimarisha mifumo ya kutambua, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya milipuko.
Dkt. Mpango amesema hayo Mei 9, 2024 Kibaha Mkoani Pwani wakati akizindua Kampeni ya Mtu ni Afya inayolenga kujikita zaidi katika huduma za kinga ikiwemo usafi wa mazingira badala ya kuwekeza kwenye tiba.

Dkt. Mpango amesema, ikiwa idara hizo zitawezeshwa zitaweza kujengewa uwezo wa kukabiliana na magonjwa ya milipuko ikiwemo kuimarisha mifumo ya kutambua, kudhibiti na kukabiliana na magonjwa.
"Endapo idara hizi zitawezeshwa licha ya kubaini na kukabiliana na milipuko pia zitaweza kufanya tafiti kuhusu magonjwa mbalimbali ili kubaini jinsi yanavyosambaa, vihatarishi na tiba yake,"amesema Dkt. Mpango.

Dkt. Mpango ameongeza kuwa endapo idara hizo zikiwezeshwa zitasaidia kujenga usimamizi na upimaji matokeo wa kampeni ya Mtu ni Afya sambamba na kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu usafi na umuhimu wa mazoezi ya viungo kupitia program za elimu mashuleni, machapisho mbalimbali na kupitia vyombo vya habari.
Aidha, ametoa rai kwa Halmashauri zote kuwatumia wahudumu wa ngazi ya jamii ambao watawezesha kufikiwa sehemu kubwa ya jamii lakini kuchochea mabadiliko ya tabia za wananchi na kubakikisha usawa na urahisi wa utoaji wa huduma.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali ya awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Afya imekuwa ikiboresha huduma za afya kwa watanzania kwa kutilia mkazo masuala mbalimbali ikiwemo huduma za Afya kinga ili kudhibiti na kuzuia magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza yanayoweza kutokea kwenye jamii.

"Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru viongozi wangu kwani mmekuwa mkiniunga mkono kwenye uanzishaji na utekelezaji wa Kampeni hizi. 

"Niwakumbushe kuwa, Kampeni ya Usafi wa Mazingira awamu ya kwanza (2012-2015) ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa wakati ule, Awamu ya Pili (2016-2022) ya Kampeni hiyo ambayo ilikuwa na kauli mbiu isemayo NYUMBA NI CHOO ilizinduliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye alikuwa Makamu wa Rais kwa wakati huo,"amesema Waziri Ummy.

Ameongeza kuwa katika kampeni hizo mafanikio makubwa yamepatikana kwenye Kampeni ya Taifa ya Usafi wa awamu ya pili ambapo taarifa ya utafiti ya viashiria vya afya uliofanywa na NBS imeonesha ongezeko la watu wanaotumia vyoo bora kutoka asilimia 21 mwaka 2016 hadi asilimia 74.8 mwaka 2022.
Kampeni ya Mtu ni Afya Awamu ya Pilli itatumia mbinu mbalimbali ambazo zitaleta mabadiliko ya tabia katika jamii ambazo zitajumuisha Televisheni, Redio na Mitandao ya Kijamii. Vilevile, Kampeni hii itaendesha uhamamsishaji kwa kutumia Wasanii maarufu hapa nchini.

Utekelezaji huu unalenga kuhamasisha jamii na taasisi zote kuhusu ujenzi na matumizi ya vyoo bora, kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kunawia mikono kwa maji tiririka na sabuni pamoja na kudhibiti kabisa tabia ya kujisaidia ovyo. 

Kampeni hii itawezesha upatikanaji wa huduma za msingi za usafi wa mazingira kwa watu wote ikiwa ni pamoja na udhibiti wa tabia ya kujisaidia ovyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news