SINGIDA-Wizara ya Fedha imepongezwa kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha vijijini ambako wananchi wengi wameathirika kiuchumi kutokana na matumizi mabaya ya fedha kutokana na kukosa elimu kuhusu matumizi ya fedha, kuweka akiba na kukopa bila kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, alipoungana na wajasiriamali na Wananchi wa Iramba mkoani Singida katika ukumbi mpya wa mikutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wialayani Iramba, kupata mafunzo ya elimu ya fedha yaliyotolewa na Wizara ya fedha kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais -TAMISEMI.
‘’Mimi nawashukuru sana Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuamua kupita kwa wananchi kuwaeleza, kuwapa elimu ya fedha,’’alieleza Dkt. Mganga.
Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bw. Salim Kimaro, alisema kuwa Wizara ya Fedha inatambua umuhimu wa elimu ya fedha hivyo itaendelea kutekeleza mpango wake wa kuelimisha watanzania wote kuhusu masuala ya fedha ikiwemo mambo muhimu ya kuzingatia kabla ya kukopa fedha, kuweka akiba ili kujikwamua kimaisha na kukuza uchumi wa nchi.
‘’Tunayo programu ya miaka mitano ya kutoa elimu ya fedha kwa umma, ambapo sasa tumejikita katika kutoa elimu ya fedha kijijini, programu hii kwa sasa imeanza ya mikoa takribani nane, na malengo yake ni kuendelea nchi nzima, elimu hii inakwenda sambamba na uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa maana ya kwamba, unampatia elimu ili atakapopata fedha aweze kuzisimamia zimsaidie kiuchumi na kusaidia uchumi wa taifa kwa ujumla,’’ amesema Bw. Kimaro.
Bi. Pauline Ali Nsangulo ni mjasiriamali aliyeshiriki mafunzo ya elimu ya fedha, ambapo aliiomba Wizara ya Fedha kuendelea kutoa elimu ya fedha kutokana na umuhimu wa elimu hiyo kwa wajasiriamali na wananchi wote kwa ujumla.
‘’Mimi naomba semina hii tuipate wakati mwingine, mimi nimefurahishwa na elimu hii,"alisisitiza Bi. Pauline.
Aidha, Samson Bernad ni mmoja wa washiriki wa mafunzo ya elimu ya fedha wilayani Iramba ambaye alikiri kunufaika na elimu hiyo hususani namna bora ya kuandaa maisha ya uzeeni kwa kutunza akiba.
‘’Tumefurahi sana kupata mafunzo haya, hasa habari ya kuweka akiba unajua tunasema, ujana ni mtaji halafu uzee ni fainali, kwahiyo kuna watu wengi hatuweki akiba na mwisho wa siku tukiwa wazee basi tunaazna kutapatapa sana, lakini kwa elimu ambayo tumepata kutoka Wizara ya Fedha, inatuandaa vijana kwa ajili ya maisha ya uzeeni."