NA GODFREY NNKO
WAZIRI wa Uchukuzi, Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amesesema,wizara kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) hadi kufikia Machi, 2024 ilifanya uchunguzi na kusajili ndege 15 ambazo zilipewa vyeti vya ubora (Certificate of Airworthiness).
Aidha, jumla ya ndege mbili ziliondolewa kwenye Daftari la Usajili baada ya kumalizika kwa mikataba ya ukodishaji.
Ndege nyingine 91 zilikaguliwa na kupewa vyeti vya ubora ili kuendelea kutoa huduma nchini ambapo ukaguzi huo umewezesha daftari la usajili wa ndege kuwa na jumla ya ndege 419.
Prof.Mbarwa ameyasema hayo leo Mei 6, 2024 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 bungeni jijini Dodoma.
"Katika kuongeza wigo wa soko la usafiri wa anga nchini kwa kuvutia mashirika ya ndege ya kimataifa kutoa huduma za usafiri wa anga pamoja na kuimarisha ushindani katika utoaji wa huduma,
"Serikali kupitia TCAA imeendelea kusaini mikataba mipya na kuipitia mikataba iliyopo ya usafiri wa Anga (Bilateral Air Services Agreements - BASA) baina ya Tanzania na nchi nyingine."
Waziri Mbarwa amesema,hadi kufikia Machi 2024, Serikali ilifanikiwa kusaini Hati za Makubaliano tano za nchi za Poland, Suriname, Algeria, Jamhuri ya Czech na Ivory Coast.
Amesema, makubaliano hayo yaliyosainiwa yanaifanya Tanzania kuwa na Mikataba ya BASA na nchi 85 ikilinganishwa na nchi 80 iliyokuwa imeingiwa hadi kufikia mwaka wa fedha 2022/23.
"Mikataba ya BASA imewezesha Mashirika 25 ya ndege za kimataifa kutoa huduma nchini. TCAA pia iliratibu shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo ambapo hadi kufikia Machi, 2024 abiria waliosafiri kwa kutumia usafiri wa anga wameongezeka hadi abiria 5,080,920."
Waziri Prof.Mbarawa amesema, idadi hiyo ni kulinganishwa na abiria 4,105,375 katika kipindi kama hicho cha mwaka 2022/23, ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 23.76.
Vilevile, amesema mizigo iliyosafirishwa imeongezeka hadi kufikia tani 27,532 ikilinganishwa na tani 23,070.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asilimia 19.33.
Ombi
Waziri Prof.Mbarawa katika mwaka wa fedha 2024/25, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.73 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amesema, kati ya fedha hizo, shilingi 114,744,476,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 2.6 ni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.