DAR-Mwenyekiti wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC),Hamad Rashid Mohamed ametangaza kung'atuka rasmi kwenye nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Licha ya kutangaza kung'atuka, Mheshimiwa Hamad ameonesha nia ya kuwania urais kupitia uchaguzi ujao 2025 huko Zanzibar iwapo wanachama wataridhia.
Ameyasema hayo Mei 29,2024 makao makuu ya chama hicho yaliyopo Buguruni wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Vile vile, amewataka wanachama kujitokeza kugombea nafasi ya uwenyekiti, kwani uchaguzi utafanyika Juni 27,2024.
"Chama hiki ni chama ambacho kinafuata demokrasia na kuna utaratibu wa miaka 10 ya kukaa madarakani kwa maana ya vipindi viwili vya miaka mitano na mimi tayari kama Mwenyekiti nimeshaongoza kwa miaka 10, hivyo ni muda sasa wa kuacha nafasi hii na kuwapisha wengine.
"Nitangaze rasmi kuwa Juni 27,2024 kutakuwa na mkutano wa uchaguzi mkuu ambao utafanyika hapa jijini Dar es Salaam, hivyo wananchi na hasa wanachama wa chama chetu wajiandae kugombea,"amesema Hamad.
Tags
Alliance For Democratic Change (ADC)
Chama cha ADC
Habari
Hamad Rashid Mohamed
Siasa za Tanzania