Huduma za mafao kwa wastaafu ni bure, epukeni matapeli-Mwaipaja

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Fedha imesema, huduma za pensheni kwa wastaafu zinatolewa bure, hivyo hakuna sababu ya mstaafu kutoa fedha ili kuweza kupewa huduma.
Hayo yamebainishwa leo Mei 13,2024 mkoani Morogoro na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia Wizara ya Fedha, Bw.Benny Mwaipaja wakati akifungua Kongamano la Elimu kwa Wamiliki wa Mitandao ya Kijamii nchini.
Kongamano hilo la siku mbili linaangazia Pensheni na Mirathi na namna bora ya kuripoti taarifa za Bajeti.

Amesema, wameendelea kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wastaafu wanapata elimu na uelewa wa kutosha kuhusu huduma za mafao ili kuepuka kuangukia katika mikono ya matapeli.

“Kwa hiyo mada tutakazotoa leo ni mbili tu,kwanza tutazungumzia masuala ya pensheni,” amesema Mwaipaja huku akifafanua kuwa, katika mada hii mtaalamu atafundisha namna ambavyo mifuko ya hifadhi ya jamii inafanya kazi na Mfuko wa Hazina.
“Katika Mfuko wa Hazina tunaweka msisitizo sana kuhusu ni mfuko wa namna gani ili ninyi mtusaidie namna ya kuzungumza na wastaafu, wastaafu wa jumla lakini wastaafu wanaolipwa pensheni zao na masuala ya mirathi na Wizara ya Fedha kwa maana ya Hazina.

"Tunapozungumzia Hazina sasa tunazungumzia Wizara ya Fedha, katika hizo pensheni kwa hiyo katika miaka ya hivi karibuni na mpaka sasa bado kuna changamoto kwamba hawa wastaafu wanasumbuliwa na matapeli.

“Sasa, tukasema kwamba badala ya kujikita tu kushughulikia masuala ya kisheria kwa kuwatafuta hao matapeli ni wa aina gani, tusisitize juu ya elimu kwanza ili iwafikie wastaafu wetu, wasiingie kwenye mtego wa kutapeliwa na hao watu ambao wamekuwa wakiwapigia simu wastaafu wakiwaomba watoe fedha kiasi fulani ili mafao yao yaweze kushughulikia, sasa tunasisitiza tena kuwa, sisi Wizara ya Fedha,huduma kwa wastaafu zinatolewa bure."
“Hakuna sababu yoyote ya mstaafu kukubali kwenda kutapeliwa, kwanza tunaamini wastaafu wetu ni wasomi, ni watu ambao wameitumikia Serikali na nchi hii kwa moyo mkubwa na wanahitaji kuwa na amani wanapofanya shughuli zao wakiwa wamestaafu.

“Kwa hiyo ninyi vyombo vya habari tunaomba mtusaidie kuwaeleza wastaafu pamoja na familia zao, kuwa Wizara ya Fedha haiombi fedha kwa mstaafu yoyote ili aweze kushughulikiwa mafao yake, hakuna kitu kama hicho,”amefafanua Mwaipaja.

Kwa upande wa mada ya pili ambayo itaangazia upande wa namna ya kuripoti taarifa za Bajeti, Mwaipaja amesema wamelenga kuwajengea wanahabari uelewa ili waweze kuifahamu na kuelewa maneno ya kitaalamu ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara wakati wa uwasilishaji wa bajeti hususani Bajeti Kuu ya Serikali.

Mwaipaja amesema, kupitia ufahamu huo utawawezesha wanahabari za mitandao kuwa na uelewa wa kuchakata kwa usahihi na kuripoti kikamilifu kwa umma ili uweze kupata uelewa wa kutosha na kuepuka maswali ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakijirudia.

"Sasa watu wengi wanafanya makosa, wanasema bajeti ya Serikali ni shilingi bilioni 49.5 ukweli? Ukishaona tu kitu kinaitwa bilioni elfu nne, elfu arobaini na tisa na kitu, ujue ni trilioni.

"Sijui kama tunaelewana? Ukishaona bilioni elfu arobaini na tisa mia tatu arobaini na tano nukta saba, wewe Mwandishi wa habari ili hiyo taarifa ifike sahihi kwa mwananchi au kwa msomaji wako, hiyo ni trilioni 49.345."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news