IFAD kuendelea kusaidia miradi ya kilimo na uvuvi Tanzania

NAIROBI-Serikali imeushukuru Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kilimo na uvuvi nchini.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, baada ya kikao kati ya Tanzania na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), kando ya Mikutano ya Mwaka 2024 ya Bodi ya Magavana (Mawaziri wa Fedha kutoka nchi wanachama) wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), inayofanyika Jijini Nairobi nchini Kenya.
Dkt.Mwamba alisema Mfuko huo umekuwa ukiendelea kusaidia miradi mbalimbali ya kilimo na uvuvi nchini kwa pande zote mbili za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar).

“Tunawashukuru kwa kuendelea kufadhili miradi ambayo imesaidia kufikia malengo yaliyowekwa na nchi kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5 (Five-year National Development Plan), Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo (Agriculture Sector Development Programme) pamoja na Program ya Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tommorrow),"amesema Dkt.Mwamba.
Dkt. Mwamba aliongeza kuwa Serikali inajipanga ili kuwasilisha miradi kupitia program mpya ya Mfuko huo inayotarajia kuanza Januari, 2025 na kuwataka sekta husika (kilimo na uvuvi) kuainisha miradi mbalimbali ya kilimo, ufugaji na uvuvi ili iweze kuingia katika program mpya ya IFAD.

“Tutaongea na wenzetu wa Sekta husika kuainisha miradi ambayo Serikali inataka iingie kwenye program mpya itakayoanza Januari, 2025 na kuiwasilisha Tume ya Mipango ili ifanyiwe uchambuzi kabla ya kuwasilishwa kwenye mfuko huo,"amesema Dkt. Mwamba.Aidha,Dkt. Mwamba alieleza kuwa kutokana na changamoto ya huduma ya fedha inayowakabili wakulima wengi nchini hasa wale wadogo, Serikali pamoja na IFAD wamekubaliana kuwa katika program mpya itakayoanza Januari, 2025 kwa kuingiza miradi ambayo itasaidia upatikanaji wa fedha kwa wakulima wadogo ili waweze kuendeleza miradi yao ya kilimo na miradi ambayo inawagusa wananchi kwa moja.Pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Dkt. Mwamba alisema kuwa ili kuimarisha sekta ya uvuvi nchini, suala la uhifadhi wa mazingira limetiliwa mkazo ili kulinda mazalia ya samaki ambayo yanaweza kuharibiwa wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Amesema,kwa kuwa program hiyo ya IFAD inahusisha uwepo wa meli kubwa za uvuvi, upembuzi yakinifu unaendelea kufanywa kuhusu kulinda mazingira ya mazalia hayo ya samaki ili wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo isiathiri sekta ya uvuvi nchini.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mshiriki anayeshughulikia miradi kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Dkt. Donal Brown, alisema IFAD kupitia miradi yake mbalimbali inalenga kuinufaisha jamii hasa kwa wale wanaoishi vijijini ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu inayohusiana moja kwa moja na kilimo cha biashara.

‘’Miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), inalenga moja kwa moja kusaidia jamii nzima zilizopo vijijini kupitia miradi mikubwa mbalimbali inayotekelezwa na Mfuko, hasusan ile ya maji ambayo inasaidia kurahisisha na kuendeleza kilimo cha kibiashara,"amesema Dkt. Brown.Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) umekuwa ukifanya kazi na Serikali ya Tanzania ili kuendeleza sekta ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini ili kufikia uzalishaji wa juu, endelevu na kibiashara. Ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya wakulima wadogo na kuboresha upatikanaji wa masoko.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news