Jaji Mkuu wa Tanzania ashiriki Maadhimisho ya Miaka 100 ya Mahakama ya Ireland

• Apata fursa ya kuteta kidogo na Rais wa Ireland

• Rais Higgins abainisha jinsi alivyovutiwa na maisha na Uongozi wa Hayati Mwalimu Nyerere

DUBLIN-Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma jana tarehe 28 Mei, 2024 aliungana na Majaji Wakuu kutoka nchi mbalimbali Duniani katika maadhimisho ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa Mahakama huru nchini Ireland.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Ireland, Mhe. Donal O’Donnell wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa Mahakama huru nchini Ireland iliyofanyika jana tarehe 28 Mei, 2024.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika Jengo la Mahakama ya Upeo (Supreme Court) lililopo Mji Mkuu wa Dublin na yalihudhuriwa na Majaji Wakuu pamoja na Marais wa Mahakama za Upeo kutoka Nchi za Wanachama wa Jumuiya ya Ulaya (European Union), Rais pamoja na Majaji wa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Jumuiya ya Ulaya. Vilevile kulikuwa na Washiriki kutoka Jumuiya ya Madola akiwemo Jaji kutoka Mahakama ya Upeo ya Uingereza, Jaji kutoka Mahakama ya Upeo ya India.
Jaji Mkuu wa Ireland, Mhe. Donal O’Donnell (aliyesimama mbele) akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya kuanzishwa kwa Mahakama huru nchini Ireland iliyofanyika jana tarehe 28 Mei, 2024.

Katika muendelezo wa sherehe hizo washiriki wote walikaribishwa katika hafla maalum iliyoandaliwa na Rais wa Jamhuri ya Ireland, Mhe. Michael Higgins ambaye wakati akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Juma alizungumzia namna ambavyo alitembelea Tanzania miaka ya 1960.

“Wakati nikiwa kijana na mwanzoni mwa maisha yangu ya kisiasa nilitembelea Tanzania, niliguswa sana na maisha pamoja na Uongozi wa Rais wa Kwanza wa Tanzania na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” alisema Mhe. Higgins huku akiongeza kuwa, Tanzania na Ireland zina historia kubwa kwa miaka mingi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis (kushoto) akizungumza jambo na Rais wa Jamhuri ya Ireland, Mhe. Michael Daniel Higgins wakati alipowasili Ikulu kwa mwaliko wa Rais huyo.

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na wageni kuzungushwa katika maeneo mbalimbali ya Mahakama hiyo pamoja na kupewa historia ya Mahakama hiyo ambapo wageni walipata maelezo ya kina kuhusiana na uanzishwaji wa Mahakama Huru nchini Ireland na baadaye kufuatiwa na sherehe iliyofanyika katika Mahakama ya Upeo.

Baada ya hapo washiriki walikaribishwa kwenye chakula cha usiku na Jaji Mkuu wa Ireland, Mhe. Donal O’Donnell katika ukumbi wa Chama cha Mawakili (Honorable Society of King’s Inns).

Maadhimisho hayo yalifanyika kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mahakama Huru za nchini Ireland mwaka 1924.

Mahakama Huru za Ireland zilianzishwa mwaka 1924 kufutia uhuru wa Ireland kutoka Ukoloni wa Muingereza na kabla ya hapo Mahakama zote za Ireland kama ilivyokuwa kwa Makoloni mengine ya Muingereza zilikuwa chini ya Sheria ya Uingereza na Maafisa wa Kiingereza.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji Wakuu wa Ireland na Ireland Kaskazini. Kulia ni Mhe. Donal O’Donnell na kushoto ni Mhe. Dame Siobhan Keegan.

Jaji Mkuu wa Tanzania yupo Jamhuri ya Ireland baada ya kutembelea Ireland ya Kaskazini kwa mwaliko wa Jaji Mkuu wa Ireland ya Kaskazini na Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Ireland ambapo pamoja na mambo mengine leo atapata fursa ya kutoa muhadhara kwenye Taasisi ya Kimataifa na Masuala ya Jumuiya ya Ulaya (Institute of International and European Affairs).
Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa akisalimiana na Rais wa Jamhuri ya Ireland, Mhe. Michael Daniel Higgins wakati wa hafla maalum iliyoandaliwa na Rais huyo jana tarehe 28 Mei, 2024.

Safari hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubalino kati ya Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) na Taasisi isiyo ya kiserikali ya nchini Ireland ya (Irish Rule of Law International), makubalino hayo yana lengo la kuwajengea uwezo Maafisa wa Mahakama kutoka Tanzania, Ireland ya Kaskazini na Jamhuri ya Ireland kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Waambata wake. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Jaji kushoto ni Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.

Mhe. Prof. Juma ameambatana na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Jaji Mfawidhi Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mhe. Mwanabaraka Mnyukwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news