Jaji Sehel atoa rai kwa majaji, mahakimu wanawake Afrika

NA MARY GWERA
Mahakama Accra

MWENYEKITI wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Barke Sehel ametoa mada katika Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika huku akiwasihi Majaji Wanawake kutoka Nchi za Ukanda huo kuwa sehemu ya kuendeleza jitihada za kuhamasisha pamoja na kuelimisha kuhusu usawa na haki za kijinsia.
Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Barke Sehel akitoa mada kwenye Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika jana tarehe 15 Mei, 2024 Accra nchini Ghana.

Akitoa mada kuhusu jinsi Mahakama ya Tanzania inavyoshughulikia Mgawanyiko wa Jinsia ‘Bridging the Gender Divide in the Judiciary of Tanzania’, jana tarehe 15 Mei, 2024 katika Mkutano huo unaofanyika Accra nchini Ghana, Mhe. Sehel alisema ni muhimu Wanawake kuendeleza majadiliano kuhusu usawa wa kijinsia.
Sehemu ya Majaji Wanawake kutoka Ukanda wa Afrika walioshiriki katika Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Barke Sehel akitoa mada ya Mgawanyiko wa Jinsia ‘Bridging the Gender Divide in the Judiciary of Tanzania’.

“Jitihada kuhusu kuwa na usawa wa kijinsia na ushirikishwaji lazima ziendelee, na sote tuna wajibu wa kuhimiza na kuwa sehemu ya mijadala kama hii ikiwa tunataka kufikia mabadiliko ya maana na kuunda fursa zaidi za haki shirikishi,” alisema Mhe. Sehel.

Akizungumzia namna Serikali na Mahakama ya Tanzania zinavyoshughulikia suala la pengo la kijinsia ndani ya Mahakama, Mhe. Sehel aliwaeleza washiriki wa Mkutano huo kuwa, jitihada mbalimbali zimechukuliwa nazo ni pamoja na kuongeza idadi ya Majaji na Mahakimu Wanawake kwa kuajiri na kuteua wale wanaokidhi vigezo.
Baadhi ya Majaji na Mahakimu Wanawake kutoka Mahakama ya Tanzania wakifuatilia Mada iliyokuwa ikitolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel (hayupo katika picha).

Aliongeza kuwa, Mahakama imekuwa ikijenga miundombinu wezeshi/mizuri inayoweka mazingira rafiki na wezeshi kuweka kuwavutia wanawake kufanya kazi ndani ya Mahakama.

“Kadhalika kumekuwa na uanzishwaji wa Mahakama maalum zinazoshughulikia masuala maalum ya kijinsia, yote hii ni katika jitihada za kupambana pengo la kijinsia,” alieleza Mwenyekiti huyo.

Akitoa takwimu za idadi ya Majaji na Mahakimu wanawake, Mhe. Sehel alibainisha kuwa kwa upande wa Mahakama ya Rufani kuna jumla ya Majaji 35 ambapo idadi ya Majaji wanaume ni sawa na asilimia 58.33 na wanawake 13 sawa na asilimia 41.67. Jaji Mkuu wa Ghana, Mhe. Getrude Sackey Torkornoo (kushoto) akimpatia zawadi Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Barke Sehel.

Kwa upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sehel aliwaeleza Washiriki wa Mkutano huo kuwa, kuna jumla ya Majaji 106 ambao kati yao wanawake ni 39 sawa na asilimia 36.79 na 67 ni wanaume ambao ni sawa na asilimia 63.21.

Kadhalika, Mhe. Sehel alieleza jitihada zilizochukuliwa na TAWJA katika kushughulikia suala la jinsia ambapo amesema ilizindua Kitabu maalum kinachogusia masuala mbalimbali ya jinsia na haki za wanawake 'Gender Bench Book'.
Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa akiwasilisha mada katika Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika kwa niaba ya Jaji Imani Aboud, Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.
Jaji wa Mahkama Kuu Zanzibar, Mhe. Aziza Suwedi akifuatilia mtoa mada (hayupo katika picha) wakati wa Mkutano wa 18 wa Chama cha Majaji Wanawake Duniani (IAWJ) Ukanda wa Afrika. (Picha na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania).

Aliongeza kwamba, TAWJA imekuwa ikishirikiana na Wadau mbalimbali ‘stakeholders engagement’ ili kutoa elimu kuhusu masuala ya jinsia na kadhalika.

Katika Mkutano huo, TAWJA pia imepata nafasi ya kutoka Mada nyingine zilizowasilishwa na Mhe. Victoria Nongwa, Jaji Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambaye alitoa kwa niaba ya Jaji Imani Aboud pamoja na kuongoza moja na mjadala wa mada ambapo uliongozwa na Mhe. Aziza Suwedi kutoka Mahkama Kuu Zanzibar.

Mkutano huo umebeba Kaulimbiu isemayo; 'Nafasi ya Majaji Wanawake katika kupambana na mila potofu katika ulimwengu wa sasa’.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news