KAGERA-Wananchi wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Fedha kwa kuwafikishia huduma ya elimu ya fedha itakayowakomboa kiuchumi na kuwaepusha na upotevu wa fedha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata elimu hiyo, Bi. Ivona Gasper Mfanyabiashara alisema kuwa elimu aliyoipata ataenda kuwaelimsha wengine ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha.
“Tunaiomba Serikali iendelee kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wake na kuhakikisha inawafikia watu wote nchi nzima kwa sababu wananchi wengi wanapoteza fedha kwa kukosa elimu,” alisema Bi. Gasper.
Mwelimishaji Rika Ngazi ya Jamii Bi. Jackline Petro, alisema kuwa baada ya kupata elimu ya fedha amejua sehemu sahihi ya kutunza fedha zake kama vile benki, saccoss mbalimbali na vikundi vidogo vidogo vilivyosajiliwa.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa Serikali itahakikisha watu wote waliokusudiwa kupata elimu awamu ya kwanza wanafikiwa kama ilivyopangwa.

Kwa upande wake Afisa Biashara Mkoa wa Kagera na Mratibu wa Huduma za Fedha ngazi ya Mkoa, Bw. Keneth Mlilo, alisema kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa wananchi kujitokeza kupata elimu ya fedha hususan kundi la kinamama kwa kuwa imeonekana kundi hilo ndilo waathirika wakubwa wa mikopo umiza yenye riba zisizolipika.