Kimbunga Hidaya kimesogea zaidi huku TMA ikitoa tahadhari na ushauri

DAR-Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa kimbunga Hidaya kilichopo katika Bahari ya Hindi mashariki mwa pwani ya nchi yetu.
Ķwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na TMA, kufikia saa 9 mchana wa leo, Kimbunga Hidaya kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 276 kutoka pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi) na kilomita 300 kutoka pwani ya Mtwara kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 981hPa na kasi ya upepo unaofika kilomita 130 kwa saa.

"Kama ilivyotabiriwa awali, uwepo wa kimbunga Hidaya karibu na pwani ya nchi yetu umeendelea kutawala mifumo ya hali ya hewa kwa baadhi ya maeneo ambapo katika kipindi cha saa 12 zilizopita, vipindi vya mvua na upepo mkali vimeanza kujitokeza.

"Mfano katika kituo cha hali ya hewa Mtwara, upepo mkali unaozidi kilomita 40 kwa saa umeweza kupimwa katika nyakati tofauti kuanzia asubuhi ya leo.

"Hali kama hiyo pia imeweza kujitokeza katika vituo vyetu vingine vilivyopo katika ukanda wa pwani kama vile vituo vya hali ya hewa vya Kilwa Masoko, Zanzibar na Pemba.

"Vile vile katika kipindi hicho, vipindi vya mvua vimeweza kushuduhiwa katika maeneo ya Mtwara na Lindi.

"Matarajio ni kwamba kimbunga Hidaya kitaendelea kusogea kuelekea karibu kabisa na ukanda wa pwani ya nchi yetu usiku wa leo na mchana wa kesho tarehe 4 Mei 2024 kabla ya kuanza kupungua nguvu yake kuelekea siku ya Jumapili tarehe 5 Mei 2024."

"Kwa usiku wa leo na siku ya kesho tarehe 04 Mei 2024, kimbunga Hidaya kinatarajiwa kusababisha matukio ya vipindi vya mvua kubwa na upepo mkali katika maeneo ya ukanda wa pwani hususan wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani na Dar es salaam pamoja na kisiwa cha Unguja.

"Vilevile, matukio ya mawimbi makubwa baharini yanatarajiwa kujitokeza katika ukanda wote wa mwambao wa pwani ya Bahari ya Hindi."

USHAURI: 

Wananchi katika maeneo tajwa na wote wanaojihusisha na shughuli mbalimbali baharini wanashauriwa kuchukua tahadhari kubwa na pia kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri na tahadhari kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

"Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga “HIDAYA” na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila baada ya masaa matatu, na mara kwa mara kila inapobidi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news