KingJada Hotel yaanza kutoa huduma Morocco Square, NHC yatoa neno

NA GODFREY NNKO

WATANZANIA zaidi ya 100 ni miongoni mwa wanufaika wa fursa za ajira kupitia KingJada Hotels and Apartments Ltd iliyopo katika jengo la Morocco Square jijini Dar es Salaam.

Mradi wa Morocco Square unamilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ukijumuisha majengo manne ikiwemo makazi,ofisi, maduka na hoteli ambayo imekodishwa.
Sanjay Madanraj Shah ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli hiyo katika uzinduzi wa awali wa KingJada Hotel ambao umefanyika Mei 23,2024 jijini Dar es Salaam amesema, safari yao ilianza mwaka 2020.

"Kwa hiyo, tupo hapa leo kwa ajili ya kufanya uzinduzi wa awali, kwa sababu, soko la utalii kwa sasa ni kubwa hapa Tanzania, kwa hiyo tumeona tuanzie hapa.

"Kuna zaidi ya wafanyakazi wazawa 100 ambao wanafanya kazi hapa KingJada."

Amesema, ajira zaidi zitafunguka ikizingatiwa kuwa wanatarajia pia kupanua matawi ya hoteli hiyo.

Hata hivyo, amesema uzinduzi rasmi unatarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu na wanatarajia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan atakuwa mgeni rasmi.

Naye Adeline Mmari ambaye ni Meneja Usimamizi wa KingJada Hotels and Apartments amesema, hamasa ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika Sekta ya Utalii inawapa nguvu ya kufanya vema zaidi.

Mmari ameipongeza NHC kwa kujenga majengo hayo ya kisasa, mradi ambao umewezesha uwekezaji wa hoteli hiyo ya kisasa.

"Na lengo letu kubwa ni kutoa ajira kwa vijana, lakini pia rika la kati la Watanzania wenzetu, kadri tunavyoendelea kupanua mradi wetu.

"Imekuwa ni fursa kubwa kuweza kuwekeza ndani ya mradi wa National Housing na tunaimani kwamba wataendelea kuwekeza katika miradi mikubwa na sisi tutapata faida zaidi huko mbeleni."

Amesema, wanatarajia kutoa huduma bora ambazo zitawapa thamani wateja wao na hawatajuta kufika tena na tena hotelini hapo.
Naye, Yohana Julius Mwaigaga ambaye ni Afisa Rasilimali Watu wa KingJada Hotels and Apartments amesema, ajira nyingi katika hoteli hiyo zitakuwa za Watanzania.

"Tumeajiri zaidi ya Watanzania 100 ambao wamenufaika na ajira kutoka idara tofauti tofauti hotelini hapa."

Pia, amesema wanajivunia kuwa eneo ambalo linafikika ambapo hoteli yao ni hadhi ya Kimataifa.

NHC

Kwa upande wake, Emmanuel Lyimo ambaye ni Kaimu Meneja Mauzo na Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) amesema,

"Sisi kama National Housing tumeandaa mazingira mazuri ya uwekezaji kwa Watanzania, ndiyo maana tumekuja na mradi huu wa Morocco Square ambao unatambulika kama mixed projects.

"Huu ni mradi ambao una majengo manne ya biashara ikiwemo jengo la hoteli, jengo kwa ajili ya makazi, jengo kwa ajili ya ofisi na jengo kwa ajili ya maduka.

"Mpaka sasa, tunafurahia kuona kwamba tumempata mwekezaji KingJada Hotel ambaye amewekeza kwenye hoteli, kwenye hili jengo la Shirika la Nyumba la Taifa.

Na vile vile kwa upande wa makazi, tumefanikiwa kuuza nyumba kwa asilimia karibu 75 na zimebaki nyumba chache tu kwa ajili ya makazi. Upande wa maduka, tumefanikiwa kupangisha maduka yote kwa asilimia 100.

Kwa upande wa ofisi, tumefanikiwa kuuza na kupangisha maeneo ya ofisi, kwa sasa zimebaki sehemu chache tu kwa ajili ya kupangisha kwenye ofisi.

Kwa hiyo,National Housing tunachukua fursa hii kuwaambia Watanzania wote pamoja na wageni wetu kuwa, waje kuchangamkia fursa hii, kwani yapo maeneo kwa ajili ya ofisi na vile vile yapo maeneo kwa ajili ya makazi yamebaki machache.

Kwa, upande wa hoteli tumemaliza, tumepata mwekezaji, kwa upande wa maduka tumefanikiwa kupangisha maduka yote."

Pia, ametoa wito kwa Watanzania na wawekezaji wengine kutumia fursa iliyopo katika shirika hilo ili kuwekeza hususani miradi ya ubia.

"Mbia anapokuja National Housing, sisi tunatoa eneo kwa ajili ya uwekezaji na mbia anatoa fedha kwa ajili ya uwekezaji. Kwa hiyo, Watanzania na wageni waje kuwekeza katika miradi ya ubia,"amesisitiza Lyimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news