Lengai Ole Sabaya sasa huru

ARUSHA-Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, DPP Silvester Mwakitalu leo amewasilisha katika Mahakama Kuu ya Tanzania masijala ya Arusha ombi la kuiondoa Rufaa Na.155 ya mwaka 2022 aliyokua ameikata dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro,Lengai Ole Sabaya na wenzake.
Rufaa hiyo ilikatwa na Jamhuri baada ya Sabaya na wenzake kushinda kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi Na.27 ya mwaka 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha mbele ya Hakimu Patricia Kisinda.

Aidha,rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo na Mahakama Kuu kuanzia Aprili 29 hadi Mei 3,2024 mbele ya Mheshimwa Salma Maghimbi,Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam aliyefika jusikiliza shauri hilo.

Akiwasilisha nia ya kuliondoa shauri hilo mbele ya Jaji Salma, Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Serkali, Akisa Mhando ameeleza,

“Mheshimiwa Jaji shauri hili limekuja kwa ajili ya kusikiliza rufaa,hata hivyo mrufani (Jamhuri) imewasilisha ombi chini ya kifungu cha Sheria Na.386 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai marejeo ya mwaka 2022,ombi letu ni kwamba Jamhuri haina nia ya kuendelea na rufaa hii dhidi ya Sabaya na wenzake,hivyo tunaomba kuiondoa hapa mahakamani.”

Baada ya uamuzi huo,Jaji Maghimbi alitoa uamuzi kwamba rufaa hiyo imeondolewa mahakamani rasmi.

Kufuatia uamuzi huo, Sabaya anakuwa hana shauri lolote linalomkabili mahakamani na anahitimisha rasmi leo safari ya kesi alizokuwa anakabiliana nazo kuanzia Juni 4,2021 alipopandishwa kizimbani mara ya kwanza.

Wakili wa Sabaya,Moses Mahuna mbele ya waandishi wa habari ameeleza kwamba, kuanzia sasa,Sabaya ni mtu huru.

Pia,kwa mujibu wa mahakama yenyewe,hana rekodi yotote ya uhalifu na hana shauri lingine lolote katika chombo chochote cha sheria,na kumfanya kumalizana rasmi na Mahakama nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news