Maandalizi ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta Tija katika Ajira (ESPJ II) yashika kasi

DAR-Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda pamoja na Kaimu Mkurugenzi Huduma za Taasisi CPA Mwanahamis Chambega leo Mei 15, 2024 wameongoza kikao kazi cha kufanya tathmini ya Taasisi kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Elimu ya Ujuzi na Mafunzo ya Stadi za Kazi zenye kuleta Tija katika Ajira (Education and Skills for Productive Jobs - ESPJ II).
Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia, Bi.Catherine Mrosso (Kulia) pamoja na Mratibu Msaidizi wa ESPJ kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Osward Rukonge wakisikiliza kwa makini taarifa ya utekelezaji wa ESPJ I.
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania CPA Mwanahamis Chambega (Kulia) akifafanua jambo kuhusu utekelezaji wa ESPJ I wakati wa kikao kazi cha maandalizi ya ESPJ II. Kushoto ni Bw. Masozi Nyirenda, Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi wa TEA.
Kikao kazi hicho kimefanyika katika ofisi za Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) zilizopo Mikocheni B, Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Mratibu Msaidizi wa ESPJ kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Osward Rukonge, Mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bi. Catherine Mrosso, baadhi ya wajumbe wa Menejimenti wa TEA pamoja na watumishi waliotekeleza awamu ya kwanza ya ESPJ katika Mamlaka hiyo.
Akizungumza katika kikao kazi hicho Bw. Rukonge amesema, TEA inajua vizuri ni nini matarajio ya Serikali katika kutekeleza ESPJ II kwa sababu ni moja kati ya Taasisi zilizotekeleza kwa mafanikio awamu ya kwanza ya ESPJ; hivyo, hii awamu ya pili ya ESPJ II ni muendelezo japo kuna baadhi ya mambo katika utekelezaji yatabadilika.

Kwa upande wa nafasi ya Taasisi katika utekelezaji wa awamu ya pili ya ESPJ II, mwakilishi kutoka Benki ya Dunia Bi Catherine amesema, wanafanya tathmini kwenye Taasisi ili kujiridhisha kuwa kuna sera, kanuni, miongozo na mifumo ambayo itawezesha programu mbalimbali kutekelezwa kwa ufanisi kama vile masuala ya usalama wa jamii na utunzaji wa mazingira, kupokea na kushughulikia malalamiko kutoka kwa wanufaika, ushirikishwaji wa jamii kwa ujumla pamoja na wadau mbalimbali wa masuala ya Elimu na ujuzi.
Akitoa taarifa fupi kuhusu utekelezaji wa ESPJ I Bw. Masozi Nyirenda amesema, TEA ilifanikiwa kutekeleza programu hiyo kwa mafanikio makubwa na pia ilibaini kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa programu za ESPJ kwenye jamii hivyo iko tayari kuboresha baadhi ya mifumo na kanuni zilizotumika wakati huo ili ESPJ II ikatekelezeke kwa ufanisi zaidi na kuongeza tija kwenye jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news