Madaba wavutiwa na faida za kiuchumi kutoka mazao ya misitu

IRINGA-Halmashauri ya Wilaya ya Madaba wafanya ziara ya mafunzo wilayani Mufindi kujionea shughuli za upandaji miti uchakataji wa mazao ya misitu na uhifadhi wa misitu na mazingira.Kwa muda wa siku mbili kuanzia Mei 7 na 8, 2024 Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba iliyopo mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia Shamba la Miti Wino wamefanya ziara ya mafunzo katika Shamba la Miti Sao Hill lengo ikiwa ni kujifunza kuhusu na uzalishaji wa mazao ya misitu.
Ziara hiyo ilihusisha kiongozi wa msafara huo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Wilman Kapenjama Ndile, Madiwani, wenyeviti na Wahifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania-Shamba la Miti Wino wakiongozwa na Mhifadhi Mkuu Glory Fortunatus, ambapo katika ziara hiyo walitembelea viwanda mbalimbali vinavyozalisha malighafi zitokanazo na mazao ya misitu.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Songea amesema kuwa ziara hiyo imefanyika kwa malengo matatu ambayo ni kujifunza kuhusu upandaji wa miti kuanzia hatua ya mwanzo mpaka uvunaji, uchakataji wa mazao ya misitu katika viwanda na manufaa yake, lakini pia kujifunza namna ya kukabiliana na changamoto za uendelezaji wa rasilimali za misitu kama vile kukabiliana na majanga ya moto wa misituni.

"Nitoe pongezi zangu kwa TFS kuhusu utoaji wa elimu ya namna ya utunzaji wa miti na mazingira kwa ujumla, lakini pia tumeona manufaa mengi ikiwa ni pamoja na makusanyo makubwa ya mapato kwa halmashauri zote mbili za Wilaya ya Mufindi na Halmashauri ya Mji Mafinga na utoaji wa ajira kwa vijana na jamii inayozunguka maeneo ya shamba zitokanazo uwepo wa mazao ya misitu," alisema Mkuu wa Wilaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mhe. Teofanes Mlelwa amesema kuwa wamejifunza mengi na kubwa zaidi ni uwepo wa kiwanda ambacho kinatumia malighafi yote ya mti ikiwa ni mabaki ya miti katika utengenezaji wa bidhaa.
"Hivyo ni imani yangu kwamba katika Halmashauri ya Madaba tutapata kiwanda kama hicho ambacho kinakusanya mabaki yote ya miti kwa ajili ya kutengenezea bidhaa mbalimbali kwa tutaendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti kwa wingi kama tulivyoona hapa kwaajili ya kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmojana taifa kwa ujumla."Amesema Mwenyekiti Halmashauri ya Madaba

Akizungumza wakati wa kuwapokea viongozi hao Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Mhe. Dkt Linda Salekwa amesema kuwa ni faraja kubwa kwao kuona viongozi kutoka halmashauri nyingine wanakujakutembelea katika wilaya yetu kwa ajili ya kijifunza juu ya manufaa ya misitu.
"Hapa kwetu tunavyo viwanda vingi vinavyochakata mazao ya misitu, lakini tunao wataalamu wengi wakiongozwa na Mhifadhi mkuu wa Shamba la miti Saohill hivyo ni matumaini yangu kwamba mtakwenda kujifunza mambo mengi zaidi yanohusu uhifadhi,"amesema Mhe. Dkt Linda Salekwa

Naye Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Wino Glory Fortunatus amesema kuwa wamekuja na viongozi kutoka halmashauri lengo ikiwa ni kujifunza na kupata uzoefu juu ya manufaa yatokanayo na uhifadhi wa misitu na wamechagua Shamba la Miti Saohill kwa kuwa ndio shamba kubwa la miti ya kupandwa hivyo anaamini kuwa wataendelea kutoa ushirikiano zaidi ili kuendeleza uhifadhi katika halmashauri ya Wilaya ya Madaba.
Akiwakaribisha Shamba la Miti SaoHill, Mhifadhi Mkuu wa Shamba, PCO Tebby Yoramu amewapongeza kwa kufanya ziara hiyo hususani katika shamba la Miti Sao Hill na kuhakikisha elimu waliyoipata wanaifikisha kwa wananchi katika maeneo yao ili shughuli za uhifadhi zifanikiwe kwa ukubwa zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news