DAR-Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke, Mheshimiwa Arnold Emmanuel Peter ameushukuru Uongozi wa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kwa kutoa mafunzo kwa watendaji na madiwani kuhusu diplomasia ya uchumi na utatuzi wa migogoro.
Mheshimiwa Peter amesema, mafunzo haya kwa waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Temeke yaliandaliwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke na yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
“Mafunzo kuhusu Utatuzi wa Migogoro katika ngazi ya Halmashauri na Manispaa na Mchango wa Serikali za Mitaa katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi ni muhimu sana kwetu sisi, tumejifunza mengi na tumeongeza maarifa ambayo yatatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa weledi,” alisema Mheshimiwa Peter.
Naibu Meya alitoa wito kuwa mafunzo haya ni vizuri yakatolewa na kwa watendaji wa Halmashauri na Kata ili waweze kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.
Kwa upande wake, Dkt. Jason Nkyabonaki, Mkuu wa Taaluma aliyemuwakilisha Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Dkt. Salim Ahmed Salim, Dkt. Felix Wandwe alisema,mafunzo hayo ni muhimu kwa madiwani.
"Hasa tukitambua kuwa nyakati hizi wasomi wameelekeza kuwa katika karne ya 21, ujinga si kutojua kusoma na kuandika bali mjinga ni yule ambaye hawezi kujifunza.
“Tumejifunza misingi ya Uongozi, dhana ya Diplomasia ya Uchumi na namna ya kutatua migogoro.
"Hatuwezi kutatua migogoro katika mazingira ya wenye njaa. Kupitia mafunzo haya waheshimiwa Madiwani naomba tuzidi kuwa pamoja, tunahitaji namna bora ya kukaa pamoja na tambueni kuwa Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ni Kituo bora na salama cha kujifunzia.
"Nachukua fursa hii, kwa niaba ya Uongozi wa Kituo kuwaomba waheshimiwa Madiwani msiishie hapa njooni CFR, waleteni pia ndugu, jamaa na vijana wenu wasome. Kituo kinatoa kozi mbalimbali tunawakaribisha kuja kuongeza maarifa.
“Nina imani waheshimiwa Madiwani baada ya mafunzo haya mtakuwa mabalozi wazuri wa kukisemea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kuwa ni kituo bora kinachotoa program za mafunzo kulingana na mahitaji ya sasa na kinatoa wahitimu wenye ueledi na mahiri wanaotambulika kitaifa na kimataifa,” alifafanua Dkt. Nkyabonaki.
Naibu Meya wa Manispaa ya Temeke, Mheshimiwa Arnold Emmanuel Peter (wa pili kushoto) akimkabidhi cheti cha ushiriki katika mafunzo yaliyoandaliwa na CFR kwa kushirikiana na Halmashauri ya Temeke, Mheshimiwa Said Hassan Fella (kulia) ambaye ni Diwani wa Kilungule wengine ni Dkt. Jason Nkyabonaki (wa pili kulia) kutoka CFR na kushoto ni Wakili Faraja Nakua, Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Temeke.
Akizungumza kuhusu mafunzo yaliyotolewa kwa madiwani, mratibu wa mafunzo Bibi Janeth Malleo alisema mafunzo haya kwa waheshimiwa Madiwani na Watendaji wa Manispaa ya Temeke yamefanyika ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Kituo kwa kushirikiana na Uongozi wa Halmashauri ya Temeke ili kuwezesha Madiwani kutekeleza kazi zao vyema za kusimamia Halmashauri lakini pia kuwawakilisha wananchi vyema katika Kata zao.
Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim kimelenga kutoa mafunzo ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi kwa watendaji wa Serikali na wadau kutoka Sekta binafsi.
Hii itasaidia utekelezaji mzuri wa Diplomasia kwa wadau wahusika ikiwemo Sekta binafsi, Wajasiriamali wa kati na wadogo katika kuchangamkia fursa za masoko nje ya nchi.