DAR-Diwani wa Kata ya Tandika iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, Uzahilu Athumani ameitaka jamii kuweka mapenzi yao ya vyama pembeni pindi linapokuja suala la maendeleo.
Uzahilu ameyasema hayo leo Mei 25,2024 alipokuwa anamalizia ziara yake akiwa na Kamati ya Maendeleo ya Kata katika Shule ya Msingi Kilimahewa, baada ya kutembelea shule tofauti za msingi katika kata hiyo.
Amesema, Mwenyekiti wa chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan alitoa maagizo kuwa, viongozi wasikae ofisini.
"Mwenyekiti wetu wa chama Samia Suluhu Hassan ametuagiza sisi viongozi tunaomsaidia serikalini tuwafuate wananchi sio kukaa ofisini kusubiri tufuatwe."
Katika kuonesha ufanyaji kazi wake wakati wa majumuisho yake na katika kutatua changamoto za wazazi waliotaka chumba cha darasa kifanyiwe ukarabati,Diwani huyo ametaka kujua idadi ya vyumba vya madarasa vyenye changamoto, ambapo gharama zake ni mifuko 50 ya saruji na kufanyika harambee huku Diwani akitoa mifuko 20.
Aidha,katika kuonesha kuwa,maendeleo hayana chama Mwenyekiti wa chama cha upinzani cha ACT-WAZALENDO, Doto Mkumba alichangia mfuko mmoja wa saruji kati ya mifuko 50 inayotakiwa kwa ajili ya kukarabati vyumba vitano vya madarasa.
Sanjari na hayo Diwani huyo aliwakaribisha wananchi wote wa kata hiyo ya Tandika siku ya Jumamosi tarehe 1 Juni, 2024 katika mkutano wa wazi wa wananchi kuelezea yote yaliyofanywa na Diwani.