DODOMA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amezindua magari yanayotumia mfumo wa umeme ikiwa ni jitihada za Serikali za kuwezesha wananchi kutumia nishati safi nchini.

"Niwapongeze wadau wetu kutoka Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa hatua hii, mtakumbuka kwamba Serikali inaendelea kutafuta mbadala wa kuwawezesha wananchi hasa wale walio na uhitaji zaidi wa nishati safi,”amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau wanaoshirikiana na Serikali kutafuta uwezekano wa kuwa na nishati safi ya uhakika ili kufikia malengo ya asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo 2034.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UNDP, Bi. Weyinmi Omanuli ameipongeza Serikali kwa hatua zinazoendelea kuelekea kuwawezesha wananchi wake katika nyanja mbalimbali kijamii na kiuchumi.

Naye, Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Bw. Cedric Marel amesema Umoja huo una imani kubwa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati kuendeleza jitihada za kuwakomboa wananchi kwa kuandaa mazingira wezeshi yanayolenga kuboresha maisha yao.
Akitoa salamu za utangulizi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema hatua ya uzinduzi wa magari yanayotumia umeme ni mwendelezo wa mpango wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
"Huu ni mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa chini ya Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi nchini."